Pantev aanza na ushindi Ligi Kuu, JKT TZ ikiendeleza rekodi mbovu

MENEJA wa Simba, Dimitar Pantev, ameanza vyema mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara na timu hiyo, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Tanzania, katika mechi iliyopigwa leo Novemba 8, 2025 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.

Mechi hiyo ni ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa Pantev, tangu atambulishwe rasmi kukiongoza kikosi hicho, Oktoba 3, 2025, akichukua nafasi ya, Fadlu Davids aliyeondoka kikosini Septemba 22, 2025 na kurejea Raja Casablanca ya Morocco.

Katika mechi ya leo, JKT ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Edward Songo dakika ya 60, akiwazidi ujanja mabeki wa Simba na kuuzamisha mpira wavuni, akipokea pasi safi ya Paul Peter.

Hata hivyo, dakika ya 63, Simba ilichomoa bao hilo kupitia kwa beki, Wilson Nangu aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea JKT Tanzania, huku Jonathan Sowah akiihakikishia timu hiyo ushindi baada ya kufunga la pili dakika ya 76.

Ushindi wa leo ni wa tatu mfululizo kwa Simba katika Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kuifunga Fountain Gate mabao 3-0, Septemba 25, 2025, kisha 3-0 mbele ya Namungo (Oktoba 1, 2025), mechi zote akiziongoza kocha msaidizi, Selemani Matola.

Simba imeendeleza ubabe dhidi ya JKT Tanzania, kwani pambano la mwisho baina ya timu hizo ambalo lilipigwa Mei 5, 2025 pia kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, ilishinda bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa kiungo wa kikosi hicho, Fabrice Ngoma.

Mbali na hilo, Simba imeendeleza rekodi nzuri dhidi ya JKT Tanzania, kwa sababu ushindi wa leo unaifanya kushinda mechi ya saba ya Ligi Kuu, huku mara ya mwisho kwa maafande hao kuibuka na ushindi ulikuwa wa bao 1-0, Februari 7, 2020.

Pantev tangu atambulishwe kikosini Simba, alianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs ya Eswatini katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Oktoba 19, 2025, huku ile ya marudiano akitoa suluhu (0-0), Oktoba 26, 2025.

Kwa matokeo ya leo, Simba inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushinda mechi zote tatu na kufikisha pointi tisa, huku kwa upande wa JKT ikishinda moja, sare nne na kupoteza moja kati ya sita iliyocheza, ikishika nafasi ya saba na pointi nane.