Dar es Salaam. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imethibitisha taarifa za kupatikana kwa mabaki ya mwili wa mtanzania Joshua Loitu Mollel (21) aliyeuwawa nchini Israel.
Joshua alikuwa miongoni mwa vijana 260 wa Kitanzania waliokwenda Israel kwenye mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya mpango wa ushirikiano wa Tanzania na Israel mwaka 2023.
Joshua na raia wengine wa mataifa mbalimbali waliuwawa wakati wa mashambulizi yaliyotokea kusini mwa Israel na miili yao kupelewa Gaza.
Hivi karibuni Serikali ya Israel ilieleza kupokea mabaki ya Joshua aliyetekwa Oktoba 7 2023 kwenye vita ya Israel na Palestina.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wizara hiyo, ubalozi wa Tanzania mjini Tel Aviv, unaendelea kushirikiana na Serikali ya Israel kukamilisha mchakato wa urejeshwaji wa mwili nchini.
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inashirikiana kwa karibu na familia katika kufanikisha mapokezi ya mwili pamoja na mazishi ya heshima kwa kijana wetu,” imeeleza taarifa hiyo.
Desemba 17 hadi 31 mwaka 2023 familia ya Joshua iliweka msiba baada ya kuona mtandaoni kipande video iliyowahakikishia kuwa Joshua ameuawa.
Mollel baba wa marehemu Joshua, alienda Israel kwa wito wa Serikali ya Israel na kurejea nchini Desemba 29 mwaka 2023 na baada ya kurejea aliwaeleza waandishi wa habari kwamba safari hiyo ilikuwa ya huzuni isiyo na matumaini.