Viongozi wa juu Chadema matatani

Dar/Bukoba. Wakati Jeshi la Polisi likitangaza kuwasaka watu wengine 10 kwa makosa ya kupanga, kuratibu na kutekeleza matukio ya vurugu, ni dhahiri kwamba safu yote ya uongozi wa juu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) itakuwa mikononi mwa jeshi hilo.

Viongozi waandamizi wa chama hicho wamekuwa wakikabiliwa na kesi mbalimbali, jambo linalowafanya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka mahakamani, huku wakikosa dhamana kutokana na makosa hayo kutodhaminika kwa mujibu wa sheria.

Viongozi wanaoshikiliwa na wanaotafutwa na Jeshi la Polisi ni Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti, John Heche, Katibu Mkuu, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu (Bara), Amani Golugwa.

Wengine ni wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho ambao ni Godbless Lema, Boniface Jacob ‘Boni Yai’ (Mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Pwani), Brenda Rupia (Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chadema) na Deogratius Mahinyila (Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema).

Mwenyekiti wa Chadema, Lissu, ametimiza miezi saba gerezani tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025 huko Mbinga mkoani Ruvuma, alikokuwa akifanya mikutano kuelimisha wananchi kuhusu kaulimbiu ya chama chake ya No reforms, No election.

Baada ya kukamatwa, Lissu alirudishwa Dar es Salaam na kufunguliwa mashtaka ya uhaini katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na baadaye shauri hilo lilihamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dar es Salaam ambako kesi inaendelea kusikilizwa.

Wakati Lissu akiwa ndani, Makamu Mwenyekiti, Heche, aliendelea kukiongoza chama hicho hadi pale shughuli za chama hicho zilipositishwa kwa amri ya mahakama kutokana na kesi iliyopo mahakamani kuhusu mgawanyo wa mali za chama hicho.

Hata hivyo, Heche alikamatwa Oktoba 22, 2025 akiwa anaingia katika viunga vya Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo Dar es Salaam, alikokwenda  kusikiliza kesi dhidi ya Lissu.

Kabla ya kukamatwa kwake, Heche aliingia kwenye mzozo na Idara ya Uhamiaji katika mpaka wa Sirari mkoani Mara, akidaiwa alivuka mpaka kinyume cha sheria, madai ambayo aliyakana.

Wakati viongozi hao wakiwa mahabusu, Jeshi la Polisi limesema linaendelea na msako mkali kuwatafuta wanaotuhumiwa kupanga, kuratibu na kutekeleza matukio ya vurugu, uporaji wa mali na uvunjifu wa amani uliotokea Oktoba 29, 2025.

Miongoni mwa watu wanaotafutwa na jeshi hilo ni viongozi wa Chadema, akiwamo Mnyika, Golugwa, Lema, Rupia, Boni Yai, Mahinyila na Hilda Newton ambaye ni kada wa chama hicho.

Kwa mujibu wa polisi, Oktoba 29 kulitokea matukio ya vurugu, uporaji wa mali, uvunjifu wa amani katika majiji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Mbeya. Pia mikoa ya Shinyanga, Geita, Songwe, Ruvuma, Mara, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa.

Mbali ya viongozi wa Chadema, wengine wanaotafutwa ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima na Award Kalonga. Yumo pia Machumu Maximilian maarufu Mwanamapinduzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia Novemba 8, 2025 na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, msako huo unafuatia uchunguzi na ushahidi uliokusanywa hadi sasa.

“Jeshi la Polisi linawataka kujisalimisha katika vituo vya polisi mara watakapoona taarifa hii popote walipo,” limeeleza jeshi hilo.

Hayo yametokea huku ukimya ukizidi kutawala miongoni mwa mamlaka za Serikali, likiwemo Jeshi la Polisi, hukusu idadi ya watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa katika matukio hayo.

Kuhusu kadhia iliyotokea Oktoba 29, Misime amesema matukio hayo yalisababisha madhara kwa binadamu, uharibifu wa mali za umma na binafsi na kuleta athari kubwa.

Mbali na athari za uhai na maisha ya watu, amesema mali za umma zilizochomwa moto, zikiwamo ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Mahakama.

Uharibifu mwingine amesema ulitokea kwenye vituo vya mabasi yaendayo haraka kutoka Kimara Mwisho hadi Magomeni na Morocco, ATM za baadhi ya benki, ofisi za serikali za mitaa, barabara za lami na zege zilizomwa moto na baadhi ya majengo ya CCM, huku magari ya umma na binafsi yakiharibiwa.

“Mali za watu binafsi ziliharibiwa na kuchomwa moto, ikiwemo vituo vya mafuta, maduka, magari makubwa na madogo. Walifanya uporaji wa mali na fedha za watu kutoka katika maeneo ya biashara,” amesema.

Polisi katika taarifa hiyo limesema waliopanga na kutekeleza uhalifu huo wamekamatwa na kuanza kufikishwa mahakamani na kwamba, likishirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama linaendelea na msako mkali kuwatafuta wengine waliopanga na kuratibu.

Jana Ijumaa Novemba 7, 2025 watu 240 akiwamo mfanyabiashara Jennifer Jovin maarufu Niffer walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na kesi ya uhaini kutokana na matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025.

Mbali ya hao, wengine 172 walifikishwa mahakamani jijini Mwanza na kusomewa mashtaka mbalimbali yakiwamo ya unyang’anyi wa kutumia silaha, kuharibu mali kwa makusudi na kufanya maandamano bila kibali.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Oktoba 29 na 30 katika maeneo mbalimbali wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza.

Vilevile, watu tisa wakazi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Njombe wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini na kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi na Oktoba 30, 2025.

Katika taarifa ya Jeshi la Polisi, limeonya mtu au kikundi cha watu wanaopanga kufanya uhalifu wa namna yoyote likisema halitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

Pia limewatoa hofu Watanzania likiwataka kuendelea na shughuli zao, huku likiwaomba kutoa taarifa pale wanapoona dalili yoyote ya uhalifu au uvunjifu wa amani mahali popote ili hatua zichukuliwe.

Kwa upande wake, Chadema kimeutaarifu umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limemkamata Golugwa, asubuhi ya leo Jumamosi, Novemba 8, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Rupia, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Golugwa anakuwa kiongozi wa tatu wa ngazi ya juu wa chama hicho kukamatwa na vyombo vya dola, baada ya Lissu na Heche.

“Kukamatwa kwa Naibu Katibu Mkuu kunamaanisha kuwa, viongozi watatu pekee kati ya sita wa juu wa chama ndio waliobaki wakiwa huru. Tumepokea taarifa zinazoonyesha kuwa wimbi hili la kukamatwa kwa viongozi na wanachama wa chama linaendelea kushuka hadi ngazi za chini, ambako baadhi yao wanalazimishwa kukiri kupanga maandamano,” inasema taarifa ya Chadema na kuongeza:

“Tunaelewa kuwa Serikali inapanga kuwafungulia viongozi wetu mashtaka ya uhaini, katika jaribio la kudhoofisha uongozi wa chama na kulemaza shughuli zake.”

Amewahakikishia wanachama wao kwamba, chama chao kinasimama imara pamoja na wananchi wa Tanzania katika nyakati za furaha, huzuni, majonzi au magumu wakiendelea na mapambano ya kudai demokrasia katika Taifa lao.

Akizungumza na Mwananchi leo Novemba 8, Boni Yai ambaye ni miongoni mwa wanaotafutwa na polisi amesema yupo tayari kujisalimisha kama ambavyo wito wa jeshi hilo ulivyoelekeza.

“Nitakwenda, sina sababu ya kukimbia, ili iweje? Nitaenda, nawasiliana na wenzangu ili twende pamoja,” amesema.

Amesema atakwenda kujisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Hilda kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Facebook, ameandika: “Siwezi kujisalimisha popote, kama kuna kosa nimetenda basi nendeni mahakamani.”

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chadema Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, Chief Adronicus Kalumuna amesema pamoja na wenzake 14 wameachiwa kwa dhamana.

Akizungumza na Mwananchi, amesema alikamatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera Oktoba 12, 2025 na kwamba wenzake walikamatwa maeneo tofauti wakamkuta yeye akiwa rumande ambako amekaa kwa takribani siku 28 kabla ya kupata dhamana jana Novemba 7, 2025.

Kalumuna amesema walipelekwa Mahakama ya Wilaya Bukoba walikoshtakiwa kwa makosa ya uchochozi.

“Tumedumu ndani kwa siku 27 wengine 28 siku ya jana tumepelekwa mahakamani kwa kosa la uchochozi kwenye uchaguzi mkuu ila baadaye tumepata dhamana na kwenda nyumbani kwetu,” amesema.

Kada wa Chadema, mkazi wa Kata Kibeta, Manispaa ya Bukoba, Revocatus Willison pia amethibitisha kuachiwa kwa dhamana mahakamani akiwa na wenzake 15.

“Ni kweli tunamshukuru Mungu tumeachiwa huru kwa dhamana na sasa hivi (alipozungumza na Mwananchi mchana) niko kanisani nikitoka nitazungumza,” amesema.

Mahakama Kuu Oktoba 23, 2025 iliamuru Jeshi la Polisi nchini, kuwaachia huru watuhumiwa saba linaowashikilia nje ya saa 24 za kisheria, akiwamo Chief Kalumuna na Revocatus.

Majaji katika uamuzi kwenye mashauri mawili tofauti walisema kutoheshimiwa kwa sheria hakuvumiliki, wakinukuu ibara ya 15(1) na (2) ya Katiba ya Tanzania inayokataza mtu kukamatwa na kuzuiwa pasipo kufuata sheria za nchi.

Amri hizo zilitolewa na majaji wawili wakati wanatoa uamuzi wa maombi ya ‘habeas corpus’ yaliyowasilishwa kortini na washitakiwa kupitia mawakili wao, Pereus Mutasingwa na Derick Zephrine waliofungua maombi kwa hati ya dharura.

Uamuzi wa maombi hayo ulitolewa Oktoba 23, 2025 na majaji Lilian Itemba na Gabriel Malata, wote wakiwa majaji wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Bukoba.

Katika uamuzi uliowekwa kwenye tovuti ya mahakama Oktoba 24, 2025, majaji hao waliamuru watuhumiwa wanaoshikiliwa mahabusu waachiwe huru au wafikishwe mahakamani si zaidi ya Oktoba 24, 2025.