Dar es Salaam. Baada ya kusogezwa mbele kwa ratiba ya kufungua taasisi za elimu ya juu kufuatia vurugu zilizotokea Oktoba 29, Serikali hatimaye imetangaza tarehe mpya ya kurejea vyuoni kwa wanafunzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyotolewa leo Novemba 8, 2025, vyuo vyote vya umma na binafsi vitafunguliwa kuanzia Novemba 17.
Awali, wanafunzi wa mwaka wa kwanza walipaswa kuripoti Novemba 1 na wanaoendelea Novemba 3, lakini ratiba hiyo iliahirishwa kwa sababu za kiusalama kufuatia vurugu hizo zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali na miundombinu.
Kwa ratiba mpya, wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanatakiwa kufika kuanzia Novemba 17 kwa ajili ya programu maalumu ya utangulizi, huku wanafunzi wanaoendelea wakitarajiwa kurejea rasmi kuanzia Novemba 24.
Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Carolyne Nombo, Serikali imewataka wanafunzi kufika kwa wakati na kuzingatia ratiba zote za kitaaluma.
“Wizara inawahimiza wanafunzi wote kufika vyuoni kwa wakati, kufuata ratiba zilizopangwa, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kitaaluma,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wameipokea taarifa hiyo kwa mitazamo tofauti wapo waliofurahia kurejea chuoni, lakini wapo pia walioeleza changamoto zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya ratiba.
Neema Mwakalobo, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema muda mrefu waliokaa nyumbani umewachelewesha kitaaluma.
“Tulikuwa tumeshajipanga kuanza masomo mapema, hivyo kusogezwa kwa tarehe kulituvuruga. Lakini kwa sasa angalau tuna tarehe rasmi. Tunategemea mambo yatakwenda vizuri na kalenda haitabadilika tena,” amesema Neema.
Kwa upande mwingine, Hamisi Rajab, mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) amesema kuchelewa kufunguliwa kwa vyuo kunaongeza gharama kwa baadhi ya wanafunzi hasa wale waliokwisha lipia makazi.
“Kuna wanafunzi walishaingia mkataba wa hosteli, nyingine zinatoza kila mwezi. Tukiendelea kukaa nyumbani ndiyo gharama zinaongezeka. Tunatumai ratiba hii itaendelea kama ilivyooneshwa,” amesema.
Wazazi nao wameonyesha maoni mchanganyiko kuhusu ratiba hiyo. Wengi wanasema kutokuwa na uhakika wa tarehe kulisababisha usumbufu wa mipango ya kifedha na maandalizi.
Josephine Mushi, mzazi wa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo cha Tumaini, amesema kusogezwa kwa tarehe kuliathiri bajeti ya familia.
“Mtoto wangu alishaandaliwa kila kitu, na tulikuwa tumempeleka Morogoro tayari. Aliporudi, ilibidi tumtumie fedha za nauli tena mara ya pili. Lakini sasa tuna uhakika ni Novemba 17, tumepumua,” amesema.
Hata hivyo, kwa baadhi ya wazazi, usalama na utulivu wa watoto wao ni kipaumbele kuliko ratiba.
“Hata kama ratiba imesogezwa, ilivyo muhimu ni usalama wa wanafunzi. Kama Serikali imejiridhisha kuwa mazingira ni tulivu, basi tunaunga mkono,” amesema Hassan Salum, mzazi wa mwanafunzi wa mwaka wa tatu.