ACT Wazalendo kuifikisha INEC kortini kudai viti maalumu, yenyewe yawajibu

Dar es Salaam. Wakati Chama cha ACT-Wazalendo kikikusudia kuifikisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), mahakamani kwa madai ya kukosea ukokotoaji wa kura uliosababisha wakakosa wabunge wa viti maalumu, tume hiyo imesema chama hicho hakikupata kura za kuwapa sifa za kupata wabunge wa viti maalumu.

Novemba 7, 2025, kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 66(1)(b) na 78(1) za Katiba ya mwaka 1977, pamoja na kifungu cha 112 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024, INEC iliteua wabunge wa viti maalumu 115 kati ya 116 wanaotakiwa kuteuliwa.

Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, ulioshirikisha vyama 18, vyenye usajili wa kudumu ni viwili pekee vilipata wabunge hao ambapo Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimepata viti viwili na CCM ikizoa 113.

Leo Jumapili, Novemba 9, 2025, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amekutana na waandishi wa habari makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam kuzungumzia suala hilo la ubunge wa viti maalumu.

Semu amesema chama chake kimefikia hatua hiyo baada ya kufanya mahesabu yake ya kura za wabunge nchi nzima na kubaini wamepata zaidi ya kura milioni 2.2, sawa na asilimia 6, hivyo walistahili kupata wabunge wanane wa viti maalumu lakini wamepokwa.

Kiongozi huyo amesema watakwenda mahakamani kudai haki yao ya wabunge wanane wanaostahili, kwa kuitaka INEC kueleza mfumo waliotumia kukokotoa na kupata wabunge hao.

 “Tutaipeleka INEC mahakamani ili itoe takwimu halisi walizotumia kukokotoa kupata viti maalumu,” amesema Semu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake ya chama hicho, Janeth Rite amesema idadi ya kura walizopata pia inahusiana na kiwango cha ruzuku ya kila mwezi ambayo chama kinapaswa kupokea.

Amesema baada ya kufanya mahesabu, chama kilibaini kinapaswa kupata zaidi ya Sh80 milioni kwa mwezi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

“Kinachoshangaza ni kwamba hakuna sheria inayoruhusu chama kupata wabunge wawili pekee ikiwa hakijatimiza asilimia tano ya kura. Tunataka Mahakama itoe ufafanuzi wa kisheria wale waliopata wabunge wawili, walipata kwa asilimia ngapi,” amehoji Rite.

Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho-Bara, Isihaka Mchinjita, amesema watawasilisha ushahidi mahakamani kuthibitisha kulikuwa na ‘upotoshaji na uovu’ katika mchakato wa ukokotoaji wa kura za wabunge wa viti maalumu.

“Ukokotoaji huo ulipaswa kuzingatia Ibara ya 78(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ambayo inatamka kuwa jumla ya wabunge wa viti maalumu ni 115 wanaogawanywa kwa vyama vilivyopata angalau asilimia tano ya kura,” amesema Mchinjita.

Ameongeza matokeo yaliyotangazwa yanaonyesha ‘dalili za kupikwa’ na kwamba chama chake hakiwezi kukaa kimya wakati haki ya kidemokrasia ikiendelea kupuuzwa katika mfumo wa vyama vingi.

Hata hivyo, akijibu madai hayo, Mwenyekiti wa INEC, Jacobs Mwambegele amesema tume haijatoa bado takwimu rasmi za kura za wabunge.

“Wanapaswa kwanza kuwasiliana na INEC kwa sababu tume bado haijatoa takwimu za kura za wabunge hizo wanazotaja wametoa wapi? tumetangaza matokeo ya urais pekee. Kura za wabunge ndizo zinazotumika katika ukokotoaji wa viti maalumu, si za urais.

“Ukweli hawajapata kura za kuwapa sifa za kupata wabunge wa viti maalumu,” amesema Mwambegele.