Hai. Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, amewataka viongozi wenye mamlaka nchini kutafakari kwa kina kuhusu matukio ya vurugu na machafuko yaliyoripotiwa kutokea wakati na baada ya uchaguzi mkuu, mwaka huu, akisisitiza haja ya kujenga upya misingi ya amani, umoja na haki katika Taifa.
Akizungumza leo, Novemba 9, 2025, wakati wa ibada ya kumstaafisha Mchungaji Solomon Massawe katika Usharika wa Gezaulole, Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Askofu Shoo amesema matukio yaliyoshuhudiwa wakati na baada ya uchaguzi yamesababisha maumivu makubwa kwa jamii, ikiwemo vifo, majeruhi na uharibifu wa mali za umma na binafsi.
Amedai hakuna sababu yoyote inayokubalika ya kuidhinisha yaliyotokea ambayo yamesababisha watu kuumizwa, kupotea na wengine kupotezwa na kuhimiza mamlaka zote kusikiliza kilio cha wananchi na kuchukua hatua stahiki na kwa wakati.
Amesema ni vyema kila kundi katika jamii likasikilizwa kwa sababu ushirikishwaji wa wote ndiyo msingi wa haki na amani ambao unaongoza katika kuwa na utawala bora, ufanisi na maendeleo endelevu katika jamii.
“Tumesikitishwa sana na matukio ambayo yametokea. Tumesikia na tumeona kwamba kulikuwa na maandamano yaliyosababisha watu kukamatwa, kupigwa, kujeruhiwa na hata kupoteza maisha. Wapo waliopotea, wapo waliopotezwa. Hili ni jambo linalohuzunisha sana,” amesema.
Askofu Shoo pia ameitaka Serikali na vyombo vyake kutafakari kwa kina kuhusu hali iliyojitokeza, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau wote katika kujenga maridhiano ya kitaifa.
“Niombe kwa unyenyekevu wote kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu, kuzihimiza mamlaka zote kutafakari sana juu ya haya yaliyotokea na sisi sote tujiulize hivi imekuwaje, tumefikaje mahali pa namna hii. Nchi yetu ya Tanzania tumezoea ni ya amani, nchi ambayo watu wanapendana, tumefikaje hapa na je, hivi ndivyo tunataka nchi yetu iendelee kuwa,” amesema Shoo.
Ameongeza kuwa, “Tulizungumza mengi kabla ya uchaguzi, muda mrefu tukionya, tukishauri lakini kwa kutosikilizwa yakatokea haya ambayo yametokea.
Amesema kama Taifa linapaswa kukaa pamoja kuzungumza, kuponya majeraha ya kisiasa na kijamii yaliyopo na kusikilizana kwa dhati, si kwa masilahi binafsi au ya kikundi fulani, bali kwa ajili ya Taifa na vizazi vijavyo.
Amesema, “Wito wangu, kwa unyenyekevu mkubwa naomba kama Taifa tukae pamoja kwa ajili ya kuzungumza, kuponya majeraha ya kisiasa na kijamii ambayo tayari yamekuwepo miongoni mwetu, kushauriana na kusikilizana na kuafikiana kwa pamoja kwa maana huko ndiko kunakoleta matunda mema ya baraka kwa Taifa letu.
Ametumia pia nafasi hiyo kuvitaka vyombo vyenye mamlaka na vya usalama kuepuka matumizi makubwa ya nguvu yanayoweza kusababisha upotevu wa maisha ya raia wananchi wasiokuwa na hatia, akisisitiza ni wajibu wa serikali na wa kila mwananchi kuulinda na kuheshimu uhai.
“Tuendelee kuiombea nchi yetu, tuombe kwa dhati na tuzingatie pale ambapo ni pa kuziacha njia zetu mbaya tufanye hivyo na tukubali roho mpya itawale ndani yetu, roho ya upendo, uzalendo na roho ambayo haioni aibu kutamka neno haki, roho inayokataa kuondoa uhai wa watu wasio na hatia, roho unayokataa machafuko na vurugu, kana kwamba hiyo ndiyo njia inayoweza kuleta amani, utulivu na maendeleo ya kweli.”
“Ukisoma historia ya mataifa, vurugu hazijawahi kuleta amani na hazijafikisha watu mahali popote. Watu wameweza kufika na kufikia jambo jema pale ambapo wamekuwa tayari kukaa wakahitaji utulivu wakasema hebu tukae nini kimetufikisha hapa, kwa nini tumefika katika hali hii, nani anafurahia hali hii na tufanye nini sasa,”amesema Shoo.
Amesema, “Mungu atusaidie sana nchi yetu iweze kurudia katika ile hali yake, Mungu ametupa nchi nzuri sana. Amani, haki, utulivu, upendano viwe ndizo tunu zetu na hizi tuzipandikize ndani ya vijana na watoto wetu na Watanzania wote,”amesema Shoo.
Akihubiri katika ibada hiyo, Msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Kaskazini, Mchungaji Deogratius Msanya amesema uvumilivu ni msingi wa kuyafikia mafanikio, na kuwataka watumishi na viongozi kuwa wavumilivu hata wanapopitia changamoto za kikazi na kimaisha.
Naye Katibu wa Dayosisi ya Kaskazini, Zebadiah Moshi amesema Mchungaji Solomon Massawe amehudumu katika nafasi hiyo kwa miaka 34, na amekuwa moja ya viongozi wabunifu aliyesaidia waumini kuanzisha miradi ya kujipatia kipato na kuwalea kiroho.