Atakaye mrithi Majaliwa | Mwananchi

Dar/mikoani. Nani atamrithi Kassim Majaliwa? Hili ni moja ya swali linalogonga vichwa vya Watanzania wengi walio na hamu ya kujua nani atakuwa Waziri Mkuu wa 12.

Katiba ya Tanzania, Ibara ya 51(2), inasema mapema iwezekanavyo, na kwa vyovyote vile ndani ya siku 14 baada ya kushika madaraka, Rais atamteua mbunge wa kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, mbunge huyo ni lazima awe anatokana na chama cha siasa chenye wabunge wengi zaidi bungeni, na kwa muktadha wa sasa, Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho chenye wabunge wengi wa kuchaguliwa kutoka majimboni.

Ni kwa msingi huo Rais Samia Suluhu Hassan, aliyeapishwa Novemba 3, kushika wadhifa huo katika sherehe zilizofanyika Uwanja wa Gwaride, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma, anatarajiwa kupeleka jina la Waziri Mkuu bungeni.

Majaliwa amehitimisha safari ya miaka 10 mfululizo akiwa Waziri Mkuu, sawa na Frederick Sumaye aliyeshika nafasi hiyo kuanzia 1995 hadi 2005. Tofauti ya Majaliwa na Sumaye ni kwamba Majaliwa amehudumu chini ya marais wawili akianza na Dk John Magufuli kisha Samia Suluhu Hassan, wakati Sumaye alikuwa chini ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, kati ya 1995 hadi 2005.

Samia, aliyekula kiapo cha kuanza safari ya miaka mitano madarakani, yupo kwenye mchakato wa uundwaji wa Serikali yake, na kibarua alichonacho ni kumpata Waziri Mkuu na baraza la mawaziri.

Sura mpya zilizoibuka kwa washindi kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, zitamfanya Rais Samia kukuna kichwa kwenye kulisuka baraza lake la mawaziri ili kutekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2025–2030.

Bila shaka, wapo waliokuwa mawaziri na naibu waziri katika Serikali iliyopita, anaoweza kuendelea nao tena, na wapo anaoweza kuwapa kisogo. Sura hizo, ukipitia wasifu wa wabunge wateule, zimekidhi vigezo kwani kila taaluma imesheheni bungeni na wametapakaa kila kanda ya nchi au mikoa.

Yote kwa yote, swali linabaki palepale, ni nani atakayekuwa kiranja wa baraza hilo la mawaziri? Wengi wanatajwa kwa sifa mbalimbali.

Vigezo vinavyoweza kuamua

Mbio za urais 2030 na uchaguzi wa ndani wa CCM mwaka 2027 ni miongoni mwa mambo ambayo wajuzi wa siasa wanaona itatoa taswira ya Waziri Mkuu ajaye.

Aidha, mshindi wa uspika kati ya Mussa Zungu na Stephen Masele unaweza kutoa mwelekeo wa Waziri Mkuu ajaye. Kwa nini?

Zungu ni mbunge wa Ilala, Dar es Salaam, na Masele anatokea Mkoa wa Shinyanga, kanda ya Ziwa yenye ushawishi mkubwa kisiasa nchini.

Ikiwa Zungu ataibuka mshindi wa uspika, hii itachochea kwamba Waziri Mkuu atatoka mikoa ya kuanzia Morogoro kwenda Dodoma, Singida, hadi kanda ya Ziwa. Lakini iwapo atakuwa Masele, Waziri Mkuu anaweza kutoka kanda ya kati au mikoa ya Kaskazini, kwa sababu Rais anatokea Zanzibar na Makamu wa Rais anatokea mikoa ya nyanda za juu kusini.

Huu si utaratibu wa kisheria wala wa kikatiba, lakini mara nyingi imekuwa ikifanyika ili kuepuka kuwa na viongozi wakuu katika kanda au eneo moja, hivyo kutawanya madaraka makubwa.

Nadharia nyingine ya uteuzi wa Waziri Mkuu inabashiri huenda akatoka kati ya makundi mawili, kijana au umri wa makamu ambaye hana malengo ya wazi ya kuwania urais mwaka 2030.

Mmoja wa viongozi waandamizi serikalini aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina anasema: “Kuna uwezekano mkubwa, Waziri Mkuu akatoka mikoa ya kuanzia Morogoro kwenda kanda ya kati au kanda ya Ziwa.

“Na kwa hali ilivyo ya nchi na kisiasa, tutapata Waziri Mkuu kijanakijana au umri uliosogea. Mimi naona atakuwa mwenye umri uliosogea ambaye hatakuwa na malengo ya kujitosa kwenye urais 2030,” anasema na kuongeza:

“Lakini kunaweza kuwa na ‘surprise’. Rais Samia yupo muhula wake wa mwisho, kwa hiyo anaweza kutushangaza, ila kwa vyovyote vile anapaswa kutuletea Waziri Mkuu asiyekuwa na makandokando, anayeweza kuwaunganisha watu na anayesikilizwa na makundi mbalimbali.”

Kiongozi huyo mwandamizi anasema: “Waziri Mkuu ajaye ni yule ambaye kwa kweli hatakuwa na ndoto za kuwa Rais 2030. Kwa hiyo, mtu atakayepokelewa ni yule ambaye baada ya miaka mitano atahitaji kupumzika. Hatutakuwa na Waziri Mkuu kijanakijana.”

Walichokisema wachambuzi wa siasa

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Lazaro Swai, anasema Watanzania watarajie Waziri Mkuu atakayewastua wengi kwani inaonekana nafasi hiyo itapewa mtu asiyeonekana na mipango ya kuwania urais 2030.

Itakuwa hivyo kutokana na kile anachoeleza, iwapo mtendaji mkuu wa Serikali atakuwa na malengo ya urais 2030, utendaji wake utajikita kwenye kujiimarisha kisiasa na kujipanga kwa mbio za madaraka, na sio kumsaidia Rais Samia.

“Bila shaka, hata washauri wa Rais waliopo sasa watakuwa wameliona au wanalitafakari hilo. Kwa hiyo, kati ya wengi wanaotajwa, mtashangaa kwa jina la pekee ambalo halikutarajiwa,” anasema mchambuzi huyo.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mchambuzi mwingine, Said Majjid, anayesema kutokana na uhalisia wa nyakati zilizopo, asitarajiwe Waziri Mkuu anayetokana na wanasiasa maarufu wanaoonekana kuwa na nia ya vyeo zaidi baadaye.

Anasema atapewa mtu ambaye atakuwa na msimamo mkali kwenye kuhakikisha anarudisha heshima na hadhi ya Serikali, imani ya wananchi kwa Serikali na chama, na atakayekuwa msaidizi wa kweli wa mkuu wa nchi, si mshindani.

“Mazingira yanahitaji mtu atakayekuwa msaidizi wa kweli na dhati wa mkuu wa nchi, sio mshindani wake. Tayari kuna tetesi za uwepo ushindani kwenye nafasi kadhaa zilizopo, sidhani kama Waziri Mkuu atapewa mtu atakayeongeza ushindani wa mbio za urais 2030,” anasisitiza.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya wananchi, wasomi, na makundi mengine katika jamii wakieleza aina ya Waziri Mkuu wanayemtaka, mtu mkali na mwenye kusimamia Serikali vizuri.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Governance Links, Donald Kasongi, anasema Waziri Mkuu ajaye ni lazima awe mkali katika kusimamia shughuli zote za Serikali kwa kuwa ndiye anayejibu hoja za Serikali bungeni.

“Yeye ndiye kiranja mkuu wa mawaziri wote, hivyo ni lazima awe mtu mwenye misimamo katika kufuatilia shughuli zote za serikali zisiyumbe, kwa sababu asipofanya hivyo, wa chini yake hawatatekeleza majukumu yao,” anasema Kasongi.

Pia anasema sifa nyingine ya Waziri Mkuu ni uchapakazi, uadilifu, uaminifu, asiye na tamaa za utajiri wa haraka, na mwenye uwezo wa kuiunganisha jamii yote ya Watanzania bila kujali dini, kabila, wala itikadi zao za kisiasa.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Erasto Kano, anasema Waziri Mkuu anayetakiwa kwa wakati huu ni yule ambaye ana uwezo wa kusimamia shughuli zote za Serikali kwa umakini na kwa ukali wa hali ya juu.

Anasema ili Serikali ifanikiwe kwenye utendaji wake, hasa katika kusimamia miradi ya maendeleo, ni lazima Waziri Mkuu, ambaye ndiye msimamizi wa shughuli zote za Serikali, awe mtu wa vitendo na si mzungumzaji zaidi.

“Tunataka Waziri Mkuu ambaye akizungumza, sauti yake inakuwa na mamlaka, na kila analolisimamia linafanikiwa kwa kiasi kikubwa, siyo mtu mpole ambaye atashindwa kusimamia majukumu yake,” anasema Dk Kano.

Aidha, anasema ni wakati mzuri kwa Rais Samia kupanga safu yake ya uongozi vizuri, ambao anajua watamsaidia kutekeleza majukumu yake ya kila siku, ikiwemo Waziri Mkuu mchapa kazi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John’s cha Jijini Dodoma, Dk Assad Kipanga, anasema wanamtaka Waziri Mkuu ambaye hana kashfa yoyote kuhusu mwenendo wake wa maisha ya kawaida na hajawahi kutuhumiwa kwa rushwa.

Anasema kiongozi huyo anatakiwa kuwaunganisha Watanzania wote, wawe kitu kimoja ili maendeleo yatakayopatikana katika awamu hii ya uongozi yawanufaishe Watanzania wote bila kujali maeneo wanayotoka.

“Bado tuna viongozi wazuri sana nchini ambao wanaweza kutuvusha kwenye hali hii tuliyonayo na kutupeleka kwenye hali nzuri zaidi. Tunamtaka Waziri Mkuu ambaye ataponya majeraha ya wananchi badala ya kuendelea kuwaumiza,” anasema Dk Kipanga.

Mfanyabiashara wa soko la Sabasaba, Jijini Dodoma, Agnes Nicolaus, anasema anahitaji Waziri Mkuu atakayesimamia haki, usawa, na amani, na kuiunganisha Taifa liwe kitu kimoja badala ya kuligawa kwa itikadi za kisiasa.

Anasema wanachotaka Watanzania ni amani ambayo inawawezesha kutoka na kufanya shughuli zao bila kuogopa wala kuwa na vitisho, na kumtaka Waziri Mkuu ajaye alisimamie hilo.

Orodha ya Waziri Wakuu wa Tanzania

1.    Kassim Majaliwa (2015–2025)

2.    Mizengo Pinda (2008–2015)

3.    Edward Lowassa (2005–2008)

4.    Frederick Sumaye (1995–2005)

5.    Cleopa Msuya (1994–1995)

6.    John Malecela (1990–1994)

7.    Joseph Warioba (1985–1990)

8.    Salim Ahmed Salim (1984–1985)

9.    Edward Sokoine (1983–1984)

10.  Cleopa Msuya (1980–1983)

11.   Edward Sokoine (1977–1980)

12.  Rashid Kawawa (1962–1977)

13.  Julius Nyerere (1961–1962)