Beki Mtanzania awania tuzo Marekani

BEKI wa Kitanzania, Jackson Kasanzu anayeitumikia Tormenta FC ya Ligi Daraja la Kwanza Marekani ameingia kwenye kitabu cha historia baada ya kuchaguliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora kijana.

Beki huyo amekuwa na kiwango kizuri kwenye ligi hiyo maarufu League One akiwa mmoja wa nyota wa kutumainiwa kwenye kikosi hicho.

Huu ni msimu wake wa kwanza kuitumikia timu hiyo aliyojiunga nayo akitokea San Diego Loyal alikokuwa nje ya uwanja kwa takribani msimu mzima akiuguza majeraha.

Akizungumzia baada ya kuchaguliwa, Kasanzu amesema ni faraja kwake kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho akiamini inaweza kumuongezea motisha ya kupambana zaidi.

“Namshukuru Mungu kwa sababu sio jambo jepesi kuchaguliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora, naamini hilo litaniongezea motisha ya kupambana zaidi na kuhakikisha natimiza ndoto zangu,” amesema Kasanzu.

Beki huyo mwenye miaka 22 Marekani amezitumikia timu tatu, mwaka 2022 alikuwa AFC Ann Arbor akacheza mechi tisa, msimu uliofuata akasajiliwa San Diego Loyal ambako alicheza mechi 19 za mashindano yote.

Msimu uliofuata hakucheza kutokana na kukumbwa na majeraha yaliyomkalisha nje msimu mzima na 2025/26 akajiunga na Tormenta ambapo hadi sasa ameshacheza mechi 24 akifunga bao moja.