Kachwele ataja visiki Ligi Kuu Canada

WINGA wa Whitecaps FC 2 inayoshiriki Ligi ya Canada maarufu MLS Next Pro, Cyprian Kachwele amesema amekutana na mabeki wengi kwenye ligi hiyo, lakini wa timu mbili wamempa ugumu zaidi.

Kinda huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars, aliyewahi kupita katika timu ya vijana ya Azam FC, huu ni msimu wake wa pili nchini Marekani baada ya kuchezea kikosi cha timu ya wachezaji wa akiba, Whitecaps FC 2.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kachwele amesema katika kumbukumbu zake timu mbili za Carolina Core na Rapids U-23 zimekuwa zikimpa wakati mgumu akikutana na mabeki wa timu hizo.

Aliongeza, ni mabeki wagumu kupitika na alipocheza nao amekuwa akipata wakati mgumu wakimnyima upenyo wa kufumania nyavu.

“Wachezaji majina siwakumbuki, lakini najua namba zao za jezi na timu tuliyokutana nayo, nimekuwa nikipata tabu kwa sababu kwanza mabeki wana nguvu hivyo kama hautumii akili unajikuta unawachezea faulo,” amesema Kachwele.

Hata hivyo, Kachwele alieleza licha ya kumaliza msimu salama ambao ulikuwa wa kushuka na kupanda akikumbana na majeraha, lakini mwisho alimaliza vizuri.

“Nimepitia kipindi kigumu cha majeraha, lakini baada ya kipindi hicho nilirudi nikiwa imara na namshukuru Mungu nikaendelea kupata nafasi na kuisaidia timu na hadi tukamaliza msimu salama.”

Ligi anayocheza Mtanzania huyo inachezwa kwa makundi matatu na chama la Kachwele liko kundi A na limemaliza nafasi ya 13 kati ya timu 29 kwenye msimamo wa ligi.