KOCHA wa Hausung, Hussein Rupia, amesema kukosekana kwa wachezaji wazoefu sio sababu ya mwenendo mbovu wa kikosi hicho hadi sasa, licha ya kukiri jitihada zaidi zinahitajika kuinusuru timu hiyo iliyopanda msimu huu wa Ligi ya Championship.
Akizungumza na Mwanaspoti, Rupia aliyeipandisha daraja timu hiyo, amesema ameamua kuendelea kupambana na vijana wenye kiu ya mafanikio hivyo, kinachoendelea kwa sasa ni upepo mbaya, kwa sababu wachezaji wanaendelea taratibu kuzoea mbinu zake.
“Siwezi kusema kukosekana kwa wachezaji wazoefu au ugeni wetu tofauti na timu nyingine ni sababu ya kufanya vibaya, ni mapema sana kwani unaweza ukaanza pia vizuri na ukamalizia vibaya, kikubwa sisi tunaendelea kupambana,” amesema.
Rupia aliongeza wachezaji alionao ndani ya kikosi hicho ni wachanga na wanahitaji muda kuzoea Championship, kwani walikotoka na sasa kuna utofauti mkubwa wa kiushindani, ingawa kwa viwango vya mmoja mmoja vinampa matumaini ya kufanya vizuri.
Timu hiyo ya Njombe imepanda msimu huu baada ya kuongoza First League msimu wa 2024-2025, ikitokea kundi A ilikokuwa na pointi 25, ilichapwa bao 1-0 na African Sports, ikachapwa mabao 2-0 na Polisi Tanzania, kisha kupoteza tena 3-1, dhidi ya Mbuni.