Mbongo apewa unahodha Morocco | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Kitanzania, Jaruph Juma anayekipiga Ain Diab inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka la Ufukweni nchini Morocco amepewa kitambaa cha unahodha kuiongoza timu hiyo.

Huu ni msimu wa pili kwa mshambuliaji huyo ambaye pia ni nahodha na kocha wa timu ya taifa ya Soka la Ufukweni (Beach Soccer). Msimu uliopita kwenye mechi 10 alifunga mabao manane.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha mchezaji huyo amesema, amepewa usinga huo hivi karibuni na hiyo ni baada ya kuonyesha muendelezo mzuri kwenye ligi.

“Ni kweli nimepewa unahodha, lakini viongozi wa timu waliona kama wamechelewa kunikabidhi kitambaa kwasababu zimesalia mechi nne za kumaliza ligi, waliona nafaa kuongoza, wenzangu wakanipatia majukumu hayo,” amesema Jaruph na kuongeza:

“Nashukuru Mungu kwa sababu hadi uongozi unanichagua ni wazi wameona kitu kwangu kwa sababu wachezaji ni wengi tena ni raia wa hapa. Waarabu wenyewe kwa nini wamenipa mimi.”

Jaruph ni Mtanzania pekee anayecheza soka la ufukweni katika ligi kuu ya Morocco akiwa mmoja ya nyota tegemeo kwenye kikosi hicho tangu msimu uliopita akiingia dirisha dogo na kupata nafasi moja kwa moja ya kuanza.

Msimu huu tayari chama hilo limecheza mechi 22 likishinda 13 na kupoteza tisa huku Jaruph akifunga mabao 15 zikisalia mechi nne kabla ya ligi hiyo kumalizika.