Namungo, Azam hakuna mbabe, kadi nyekundu zatawala

MECHI ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji, Namungo ‘Wauaji wa Kusini’ dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, imemalizika kwenye Uwanja wa Majaliwa Lindi, huku kukiwa hakuna mbabe baada ya miamba hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1.

Azam ilitangulia kupata bao kupitia kwa Idd Seleman ‘Nado’ dakika ya 14, baada ya kupiga shuti kali lililomshinda kipa, Mussa Malika huku ‘Wauaji wa Kusini’ wakichomoa dakika ya 52, likifungwa na Mkongomani Fabrice Ngoy.

Kabla ya pambano hilo kwenda mapumziko, ilishuhudiwa kadi mbili nyekundu zikitolewa na mwamuzi, Tatu Malogo wa Tanga, ambapo nahodha wa Namungo, Hamis Mgunya na beki wa Azam, Yeison Fuentes walitolewa nje kutokana na kusababisha mzozo.

Hata hivyo, Namungo ilishindwa kutumia vyema nafasi ya kupata bao la pili, baada ya nyota wa kikosi hicho, Lucas Kikoti kukosa penalti dakika 75, kufuatia mshambuliaji, Heritier Makambo kufanyiwa madhambi akiwa eneo la hatari na Yoro Diaby.

Hii inakuwa ni sare ya pili mfululizo ya Ligi Kuu Bara kwa Azam msimu huu baada kufungana pia bao 1-1, dhidi ya maafande wa JKT Tanzania, Oktoba 1, 2025, huku ikishinda mechi moja tu ya ufunguzi na Mbeya City ya mabao 2-0, Septemba 24, 2025.

Pia, ni sare ya pili mfululizo kwa timu hizo, kwani mara ya mwisho zilipokutana kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi zilifungana bao 1-1, Februari 27, 2025, Azam ikifunga kupitia kwa Gibril Sillah, huku Hamis Khalifa Nyenye akiifungia Namungo. 

Azam iliingia katika pambano la leo ikiwa na rekodi nzuri kwenye Uwanja wa Majaliwa, kwani mara ya mwisho ilipotembelea uwanjani hapo ilishinda bao 1-0, lililofungwa na nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda, mechi ikipigwa, Oktoba 3, 2024.