Simulizi ya mizimu ya mganga na mauaji ya muuguzi mstaafu KCMC-3

Moshi. Simulizi ya jana ya mauaji ya muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, tulisoma namna mganga wa jadi, Omary Mahmoud Rang’ambo, alivyomnywesha dawa zisizojulikana muuguzi huyo na kumfanya awe dhaifu.

Lakini mbali na kuwa dhaifu, Patricia ambaye baadaye aliuawa na mganga huyo na kumzika, kisha kumhadaa mtoto wake, Wende Mrema, kuwa amechukuliwa na mizimu, aliendelea kutapika mfululizo.

Leo tunaendelea na simulizi ya ushahidi wa Wende alioutoa mbele ya Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, ambao, pamoja na ushahidi mwingine, ulimtia hatiani Omary na akahukumiwa adhabu ya kifo.

Mauaji hayo yalitikisa mji wa Moshi na vitongoji vyake, hasa ikizingatiwa kuwa awali miongoni mwa waliokuwa wanashikiliwa kwa mahojiano ni pamoja na mtoto wa marehemu, Wende Rick Mrema, ambaye ilionekana baadaye hakuhusika.

Ni mauaji yaliyotokea tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2021 katika eneo la Rau Mrukuti, nje kidogo ya mji wa Moshi. Awali ilidhaniwa kuwa marehemu yuko India kwa matibabu, lakini baadaye iligundulika kuwa aliuawa na kuzikwa pembeni ya nyumba yake.

Mwili wake ulifukuliwa Januari 9, 2022, ikiwa ni baada ya mwaka mmoja kupita. Ndani ya shimo alipozikwa, kulikutwa pia jambia (sword) lililotumika katika mauaji, shuka lililotumika kufunika mwili wake na brassier ikiwa kifuani mwa marehemu.

Mtoto alivyomsikia mama akigugumia

Wende, aliyekuwa shahidi wa sita wa Jamhuri, katika ushahidi wake alieleza namna mama yake alivyoendelea kutapika baada ya kupewa dawa kwa nguvu na mganga huyo, Omary, ambaye sasa amehukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Wakati mama yake akiwa katika hali hiyo, shahidi huyo alisema mganga huyo alimwamuru kuondoka hapo alipokuwa na kwenda chumbani kwake ili yeye (Omary–mganga) abaki na mama yake ili amuuguze vizuri.

Akiwa chumbani kwake, shahidi huyo alisema alimsikia mama yake akigugumia, na alipomuuliza Omary kwa nini mama yake yuko katika hali hiyo, alimjibu kuwa anaharisha vitu kama shanga (beads).

Mganga huyo alimwambia kuwa anagugumia kwa sababu dawa aliyompa ilikuwa inaanza kufanya kazi, hivyo baada ya muda atatulia. Lakini Wende alimwomba mganga huyo kuona hizo shanga, akakataa na kusema mizimu itafanya kazi yake.

Mganga alivyoomba ndoo, shoka na jambia

Kulingana na ushahidi, baada ya muda hali ilitulia na kukawa kimya. Omary alimwambia kuwa waondoke hapo ili wamwache mama yake peke yake apumzike. Alipoomba ampe mama yake chakula, mganga alikataa.

Badala yake, alimtaka shahidi huyo abakie chumbani kwake na aendelee kumuombea, wakati yeye (Omary) akiendelea kumwangalia. Wakati huo ilikuwa imeshafika saa 9:00 alasiri, kwa mujibu wa ushahidi wa Wende.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa baadaye mganga huyo alimtaka ampe two mbili, jembe, shoka na jambia, wakati huo hali ya mama yake ikiwa imebadilika.

Mganga huyo alimwambia kuwa sababu ya kuomba vitu hivyo ni kwamba anataka kusafisha eneo hilo kwa ajili ya mizimu yake, ili kumwezesha kufanya kazi yake vizuri kwa sababu hali ya mama yake ilizidi kuzorota kadri muda ulivyopita.

Kwa mujibu wa Wende, aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa alimtaka aendelee kubakia chumbani kwake na asiwe anauliza maswali mengi.

Mganga huyo alimwita tena shahidi huyo na kumwagiza amletee nguo nyekundu, shuka la kimasai na sufuria, lakini akamwambia vitu hivyo lazima vikanunuliwe mjini, naye (Wende) asingeweza kumwacha mama yake peke yake.

Mganga huyo alimwambia kuwa mizimu ya kike inamwangalia mama yake, hivyo asiwe na hofu yoyote. Baada ya kauli hiyo, shahidi huyo alikwenda mjini na kununua vitu alivyohitaji na kumkabidhi Omary, ambaye alivipeleka chumbani kwa mama yake.

Alipoenda huko, mganga huyo alimwambia kuwa mama yake amepoteza fahamu, na shahidi huyo alianza kulia na kumuuliza mganga nini kimetokea. Omary akamtaka asiendelee kulia kwani mizimu itamsaidia mama yake, hivyo asihofu.

Wende aliieleza mahakama kuwa baada ya muda mfupi, mganga alimtaka ampe nguo za mama yake ili mizimu imbadilishe nguo alizokuwa amevaa ili imhamishe kwa ajili ya matibabu. Alimwambia nguo hizo zipo chumbani kwa mama yake.

Mganga huyo alimwambia aingie kwenye chumba cha mama yake, achukue nguo haraka na kuondoka, kwa kuwa mizimu imekizingira chumba chote. Alipoingia, aliona kitanda cha mama yake kikiwa kimefunikwa kwa nguo nyeupe.

Wende alisimulia kuwa mganga alimwambia hali ya mama yake ni mbaya kwa sababu amepoteza fahamu, na akamtaka aendelee kumuombea wakati yeye akihangaika kuokoa maisha yake.

Shahidi huyo aliingia na kuchukua madela mawili, kitambaa (scarf), chupi na sidiria na kumpa Omary, kisha akarudi chumbani kwake na kumwacha mganga huyo akiwa amesimama mlangoni akisoma vitabu mbalimbali.

Mama atolewa ili akabidhiwe mizimu

Wende aliendelea kueleza kuwa baadaye mganga huyo alimwambia anatakiwa awe jasiri na amsaidie kumtoa mama yake nje ya nyumba ili mizimu ianze mchakato wa kumsogeza, na wakati huo ilikuwa imeshafika saa 5:00 usiku.

Mganga huyo alimtaka Wende kuzima taa zote ili wambeba, na alimwambia Wende kumbeba miguuni pamoja na godoro, wakati yeye (Omary) angembeba upande wa kichwani na kumtoa nje ya nyumba.

Wakati wote huo, shahidi huyo alisema alikuwa anaamini mama yake yuko hai.

Mganga huyo alimwelekeza njia ya kuelekea makaburi ya familia yaliyokuwa karibu na nyumba yao. Kulikuwa na mbalamwezi, na walimchukua hadi umbali wa kama mita 20. Majirani walikuwa mbali na kulikuwa na giza licha ya mwezi.

Eneo hilo limezungukwa na miti, ambapo Omary alimwamuru shahidi huyo kurudi alipotoka na amwache yeye na mizimu, akamwagiza kuwa wakati anarudi asitazame nyuma hadi atakapofika nyumbani, azime taa zote na asubiri chumbani.

Wende aliieleza mahakama kuwa Omary ndiye pekee alibakia na mama yake. Baada ya muda kupita, kukawa kumepambazuka, ndipo aliposikia dirisha la chumba chake likigongwa na sauti ya Omary ikisema: “Tumerudi na tayari tumefanikiwa kumsafirisha mama yako.”

Omary alimwambia Wende asitoke nje ya chumba chake mpaka atakapompa amri ya kufanya hivyo, na alimuona akitundika nguo zake alizokuwa amevaa usiku ule.

Kwa mujibu wa Wende, ilipofika asubuhi, Omary alisafisha mazingira ya nyumba kwa maji, kisha kumwambia Wende kuwa anataka kuingia katika chumba cha mama yake. Wende alipokuja kuingia, alikutana na harufu ya ubani.

Akiwa anamchungulia kupitia dirishani, kwa kuwa alimwamuru asitoke nje, alimuona Omary akiwa amebeba ndoo ambayo mama yake aliitumia kutapikia jana, na baada ya hapo alimruhusu kuingia chumba cha mama yake akisafishe.

Usikose kusoma mfululizo wa simulizi hii katika gazeti letu la kesho…