Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Mohamed Kawaida amewataka wanasiasa nchini kuacha kutoa matamko, kauli au kejeli zenye kuligawa Taifa badala yake wajenge umoja, mshikamano na kudumisha amani chini.
Msimamo huo unakuja kufuatia kauli za baadhi ya wanasiasa kutoa matamko kuhusu maandamano ya Oktoba 29,2025 wakati wa uchaguzi mkuu, ambapo kulikuwa na vurugu zilizosababisha uharibifu wa mali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Novemba 9,2025 katika mkutano na waandishi wa habari, Kawaida amelaani matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29 na 30, 2025 katika maeneo mbalimbali nchini.
“Natoa rai kwa wanasiasa wenzangu, ndani ya chama changu na wale wa vyama vingine, kuacha maneno ya kejeli au matamko yenye kutoa taharuki au kutugawa. Huu ni wakati wa Taifa kuwa na umoja na mshikamano, kila mwanasiasa achunge ulimi wake, kwa sababu maneno hubomoa na maneno hujenga,” amesema Kawaida.
Kufuatia kauli hiyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Prince Mwaihojo amesema CCM ndiyo inayoongoza nchi hivyo inapaswa kusimamia amani ya nchi kikamilifu.
“Ukijaribu kuangalia yale maandamano utajua chanzo cha vurugu ni nini, ubabe katika kutafuta suluhu ya jambo, haki ni muhimu katika kutafuta amani,” amesema.
Kauli ya kawaida inakuja siku moja tangu Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi kueleza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kurejesha utengamano katika nchi na kuhakikisha wananchi wanaishi katika utawala wa sheria.
Dk Nchimbi alitoa kauli hiyo alipomwakilisha Rais Samia katika mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
“Dhamira ya Rais Samia ni kuhakikisha mchakato wa mazungumzo ya maridhiano unafanikiwa, ili kuwa na Taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na duniani kwa ujumla,” amesema.
Kawaida ameeleza kuwa vurugu hizo, ambazo kwa mujibu wake “hazikuwa maandamano halali,” zilisababishwa na vijana waliopotoshwa kupitia mitandao ya kijamii na watu wanaoishi nje ya nchi, ambao walichochea ghasia huku wakiwa salama nje ya Tanzania.
“Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya vijana wetu wakiingia barabarani kwa kushawishiwa na watu wasiokuwa na nia njema na nchi yetu, wengine wanaishi nje ya Tanzania, hawapo tena hapa, lakini wanawatumia vijana wetu kama nyenzo za vurugu na uharibifu,” ameongeza.
Kawaida amesema vurugu hizo zilisababisha madhara makubwa kiuchumi, zikiwemo biashara kusimama katika jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine, wafanyabiashara kupata hasara na huduma za kijamii kama zahanati na vituo vya polisi kuchomwa moto.
Kiongozi huyo amesema vijana walioshiriki katika vurugu walipoumia walishindwa kupata huduma za kwanza kwa sababu zahanati walizozichoma ndizo walizokuwa wanategemea kupata matibabu, jambo ambalo kwao ilikuwa hasara na kwa Taifa pia.”
“Athari za vurugu hazikubaki Tanzania pekee, bali zimeathiri biashara za kikanda kwa nchi jirani kama Kenya, Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda, Uganda na Congo, ambazo hutegemea Bandari ya Dar es Salaam kwa usafirishaji wa bidhaa muhimu,” amesema.
Mwenyekiti huyo wa UVCCM amewasisitiza vijana kutambua umuhimu wa amani, akisema kwamba maendeleo, ajira na ustawi wa Taifa haviwezi kupatikana katika mazingira ya vurugu.
“Amani si udhaifu ni nguvu ya kuleta maendeleo endelevu, vijana mnapaswa kufikiria wazee wanaohitaji dawa hospitalini, wajawazito wanaohitaji huduma au mfanyabiashara mdogo anayepata riziki yake kila siku, vurugu zinaharibu maisha ya wote hawa,” amesema.