Uzalishaji wa pareto waongezeka | Mwananchi

Mbeya. Licha ya uzalishaji wa pareto kuongezeka, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya imesema bado mahitaji ya zao hilo ni makubwa huku ikielezea mipango na mikakati ya kuhakikisha wakulima wananufaika nalo.

Wilaya ya Mbeya kwa kipindi cha miaka mitatu imeongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 2,200 hadi kufikia 3000, huku bei ikifika Sh3,500 kwa kilo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 9, 2025, Ofisa kilimo na uvuvi wa Halmashauri hiyo, Gidion Mapunda amesema licha ya kuwa wazalishaji wakubwa nchini, bado hawajakidhi mahitaji kutokana na umuhimu wa zao hilo.

Amesema katika mkakati wa kuhakikisha kiwango kinaongezeka na wanaendana na kasi iliyopo, Serikali imeanza kuzalisha miche na kuigawa bure kwa wananchi huku wakiendelea kufanya utafiti zaidi kwa kushirikiana na wadau wa zao hilo na sekta nyingine.

“Uzalishaji kwa sasa ni wastani wa tani 3,000 kutoka 15,000 kwa miaka mitatu nyuma, lakini bei kwa kilo moja ni Sh3,500, kwa maana hiyo utaona juhudi zilizofanyika na tunaendelea kushirikiana na wadau.

“Mahitaji kwa sasa ni kupata kampuni nyingi za kununua ili kuleta ushindani, kwa kuwa tulianza na mbili na sasa ni nane, tunafanya jitihada kubwa tukishirikiana na Kituo cha Utafiti Tari Uyole na wadau wengine,” amesema Mapunda.

Amesema suala la bei si kilio tena kwa wakulima, kwa kuwa uhakika wa kuuza upo isipokuwa wanahamasisha zaidi kuongeza kasi ya uzalishaji kukidhi mahitaji ndani na nje ya nchi na kujiinua kiuchumi.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo, Julius Jailos amesema pamoja na gharama kubwa zinazotumika kuandaa kilimo cha pareto, lakini wanaishukuru Serikali kuweka mazingira ya uhakika ya soko.

Amesema Serikali iendelee kuwasimamia wanunuzi kuhakikisha wanakidhi vigezo na kutofanyia biashara shambani badala yake, kuwepo utaratibu wa wafanyabishara kusubiri kukauka kwa mazao hayo.

“Tunaishukuru na kuipongeza halmashauri yetu kwa kazi kubwa ya kutupambania kupata soko, ila waangalie pia baadhi ya wanunuzi wasifuate mzigo shambani, bali wafuate utaratibu,” amesema Jailos.

Charles Munga amesema pareto imekuwa mkombozi kwenye familia na maisha yake.

Amesema kila msimu wa mavuno kwa sasa, kunakuwa na ongezeko la bei, hali inayochochea hamasa ya watu kuendelea kulilima.

“Changamoto hazikosekani katika shughuli yoyote, lakini tumeona matunda ya kilimo kwa kuwa tunahitaji zaidi soko na hili limetuongezea ari na morali kupenda kilimo chetu kwakuwa kimebadilisha maisha,” amesema Munga.