Uzoefu, ukongwe bungeni kumbeba Lukuvi kuongoza uchaguzi kiti cha Spika

Dodoma. Wakati joto la uchaguzi wa Spika wa Bunge la 13 likizidi kupanda ndani ya vyama vya siasa, Mbunge wa Isimani, William Lukuvi anatarajiwa kuongoza kikao cha wabunge watakapomchagua Spika mpya wa Bunge la Muungano wa Tanzania, iwapo atakuwepo ukumbini siku ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2023, Sehemu ya Tatu Kanuni ya 9(5), endapo Lukuvi atakuwepo katika ukumbi wa Bunge wakati wa uchaguzi, hatakuwa na mpinzani wa kukalia kiti hicho cha mwenyekiti wa kikao, kutokana na kuwa ndiye mbunge mwenye sifa zinazohitajika zaidi kwa mujibu wa kanuni hizo.

Kanuni hizo zinaelekeza kuwa uchaguzi wa Spika unasimamiwa na mwenyekiti ambaye ni miongoni mwa wabunge waliokaa bungeni kwa muda mrefu mfululizo na asiwe mgombea wa nafasi hiyo, baada ya kualikwa na Katibu wa Bunge kufanya hivyo.

Lukuvi, aliingia bungeni mwaka 1995, ndiye mbunge mkongwe zaidi miongoni mwa wabunge wa Bunge la 13, na hata katika Bunge lililopita hakukuwa na mbunge aliyemzidi kwa muda wa utumishi.

Hii itakuwa ni mara ya tatu mfululizo kwa mbunge huyo wa Isimani, mkoani Iringa, kuongoza kikao cha uchaguzi wa Spika.

Mara ya kwanza ilikuwa Novemba 10, 2020, wakati Job Ndugai (marehemu) alipochaguliwa kuwa Spika wa sita wa Bunge la Muungano na mara ya pili, Februari Mosi, 2022, wakati Dk Tulia Ackson alipochaguliwa kushika wadhifa huo.

Kwa sasa, mchuano wa kuwania kiti cha Spika ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) umebaki kati ya mbunge wa Ilala, Mussa Zungu na mbunge wa zamani wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Stephen Masele.

Vyama vingine vya siasa vinatarajiwa kutangaza majina ya wagombea wao kati ya leo na kesho.

Kwa upande wa kiti cha Naibu Spika, Kanuni za Bunge zinaeleza kuwa uchaguzi wa nafasi hiyo hufanyika baada ya wabunge wote kula kiapo cha uaminifu na hufanywa chini ya Spika aliyepo madarakani.

Wanaowania nafasi hiyo ni Timotheo Mzava (Korogwe Vijijini), Daniel Sillo (Babati Vijijini) na Najma Giga (Viti Maalumu).

Uchaguzi wa Spika unafanyika kwa mujibu wa Ibara ya 86(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotaja kuwa uchaguzi huo hufanyika wakati wowote katika mkutano wa kwanza wa Bunge jipya, au mara tu baada ya kutokea nafasi wazi katika wadhifa wa Spika.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna tarehe rasmi iliyotangazwa na Bunge kuhusu siku halisi ya uchaguzi huo. Vyanzo kutoka kwa baadhi ya wabunge wateule vinaeleza kuwa kura zinatarajiwa kupigwa Jumanne, Novemba 11, 2025, huku siku ya Jumatatu, Novemba 10, ikitarajiwa kutumika kwa ajili ya majaribio ya kiapo na ukamilishaji wa usajili wa wabunge.

Katika maandalizi ya uchaguzi huo, Katibu wa Bunge anatarajiwa kupokea majina ya wagombea wa kiti cha Spika kutoka vyama vyote vyenye dhamira ya kushiriki, ifikapo Novemba 10, 2025.

Hivyo, vyama vinapaswa kukamilisha mikutano yao ya ndani mapema ili kuteua mgombea wao rasmi.

Wakati wa usajili unaoendelea Dodoma, wagombea wanaotajwa, akiwamo Masele na Zungu, wameonekana wakizungumza na wabunge wenzao, hatua inayoelezwa kuwa ni jitihada za kutafuta uungwaji mkono.

Kwa upande wa nafasi ya Naibu Spika, Daniel Sillo na Najma Giga ndio wanaoonekana zaidi katika viwanja vya Bunge zinakofanyika shughuli hizo za usajili.

Kwa upande mwingine, historia ya Spika wa Bunge la Muungano imeonesha kuwa wengi waliowahi kushika wadhifa huo walikuwa na uzoefu mkubwa wa kibunge na kitaasisi.

Spika wa kwanza, Adam Sapi alikuwa mbunge wa muda mrefu alipopewa madaraka hayo, akafuatiwa na Pius Msekwa, aliyekuwa na takribani miaka 30 ya uzoefu.

Wengine waliokuwa na uzoefu huo ni Samuel Sitta na Anne Makinda, huku Job Ndugai alipata uspika akiwa ametumikia ubunge kwa miaka 15, na Dk Tulia akiwa na miaka saba tu ya ubunge.

Swali ambalo linaendelea kuibuka sasa ni: Je, atakayechaguliwa kuwa Spika wa nane wa Bunge la Muungano atakuwa na uzoefu wa aina gani?