Dodoma. Wabunge wateule wa Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Jumapili Novemba 9, 2025 wamekutana kwa ajili ya kumchagua mgombea uspika kupitia chama chao.
Wabunge wamekutana katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention huku kukionekana kuwa na mchuano mkali kutoka kwa wagombea na wapambe wao walioonekana kujipanga kwenye lango dogo la kuingilia ukumbini hapo.
Wanaogombea kwenye nafasi hiyo ni aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge la 12, Mussa Zungu ambaye ni mbunge wa Ilala na Stephen Masele aliyewahi kuongoza Jimbo la Shinyanga Mjini.
Kabla ya majina hayo kuchomoza, wagombea katika kiti hicho alikuwamo Spika aliyemaliza muda wake, Dk Tulia Ackson na Peter Frank.
Hata hivyo, Dk Tulia alijiondoa katika mtanange huo na jina la Peter halikuchomoza katika vikao vya chama ndiyo sababu ya kubaki majina mawili.
Kama wabunge wateule wa CCM watashiriki wote kwenye uchaguzi huo, wanapaswa kuwa 374 kwa idadi kuwa chama hicho kimeshinda majimbo 261 kwa Tanzania Bara na Zanzibar, ACT –Wazalendo wakiibuka na majimbo manane, Chaumma kikipata jimbo moja na majimbo mawili hayajafanya uchaguzi wake.
Idadi ya wabunge wa viti maalumu ambao chama hicho kimepata ni 113 kati ya wabunge 115 walioteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) baada ya viti viwili kuchukuliwa na Chaumma.
Wagombea walifika mapema katika eneo la Ukumbi wa Jakaya Kikwete na kuanza kuzungumza na wajumbe ingawa muda mfupi baadaye Zungu hakuonekana eneo la karibu na lango la kuingilia lakini Masele alibaki muda wote akipokea wabunge waliokuwa wanaingia hapo hadi alipotakiwa kuingia ndani ya ukumbi.
Mbali na uchaguzi wa Spika, wabunge hao wateule wanamchagua pia mgobea wao wa unaibu Spika ambao Kamati Kuu chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan amewapitisha Najma Giga, Daniel Sillo na Timotheo Mzava.
Kwa mjibu wa ratiba, Bunge la 13 litaanza Jumanne hii ya Novemba 11, 2025 kazi ya kwanza ni uchaguzi wa Spika ambao washindi wa leo wa CCM wanakwenda kuchuana na wale watakaopitishwa na vyama vingine kwenye nafasi hiyo.