Wakulima wasimulia maji ya bahari yanavyotafuna mashamba Pwani ya Hindi

Dar es Salaam. Tanzania inaendelea kukabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hali inayosababisha maji ya bahari kuongezeka na chumvi kuingia kwenye mashamba, jambo linalohatarisha ustawi wa kilimo na maisha ya wananchi wa pwani.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NCCS 2021–2026), Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizo katika hatari kubwa ya kukumbwa na athari za tabianchi, ikiwamo mabadiliko ya misimu, ukame wa mara kwa mara, mafuriko, upepo mkali na kuongezeka kwa kina cha bahari kunakosababisha maji ya chumvi kupenya ardhini.

Katika Kisiwa cha Mafia, athari hizo zimekuwa dhahiri katika vijiji vya Kibada na Kungwi, Kata ya Baleni, ambako bonde lililotumika kwa kilimo cha mpunga limeharibiwa vibaya na maji ya chumvi.

Mkulima Mussa Mahadhi anasema hali hiyo imepunguza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa mpunga kutokana na ardhi kupoteza rutuba.

“Awali kila mkulima alikuwa na shamba kubwa lenye mazao mengi, lakini sasa sehemu kubwa imejaa chumvi, na tija ya mavuno imeshuka sana,” anasema Mahadhi.

Ofisa Mtendaji wa Tarafa ya Kaskazini Mafia, Paul Kiyeyeu, anasema zaidi ya asilimia 20 ya ardhi yenye rutuba kwa shughuli za kilimo imeathiriwa na maji ya chumvi.

“Kilimo kinaweza kufikia ukomo katika eneo hili na vijiji jirani vitakosa maji safi endapo hatua za haraka hazitachukuliwa,” anasema huku akisisitiza haja ya kuunga mkono wakulima kupitia miradi ya kukabiliana na tabianchi.

Katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, mkazi wa Kiongwe Kidogo, Ally Masika, anasema juhudi za wanakijiji kuzuia maji ya chumvi hazijazaa matunda.

“Tumejenga kingo mara tatu, lakini mawimbi yamezidi kuwa makali na maji yanavuka, hivyo ukubwa wa mashamba unapungua kila siku,” anasema.

Rashid Makame Nchinji, mkazi mwingine, anasema ujenzi wa ukuta wa kuzuia maji chumvi ulifanywa bila kuwashirikisha wakulima, jambo lililowatia wasiwasi huku njaa ikiongezeka.

“Tulichotaka ni suluhisho la kudumu, si mradi unaoishia bila matokeo,” anasema Makame.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mafufuni, Mahadhi Mjumbe Haji, anasema hali imezidi kuwa mbaya kutokana na mabadiliko ya tabianchi na shughuli za kibinadamu kama uharibifu wa mikoko.

“Wananchi wengi wamehama maeneo yao, na hata kingo zilizojengwa hazijazuia maji kuingia,” anasema.

Katika bonde la Tondooni, Wilaya ya Mkoani, Pemba Kusini, mkulima Mohamed Fakhi anasema mimea ya mpunga inakauka mara tu maji ya chumvi yanapofika shambani.

“Nimepanda mara tatu mfululizo bila mafanikio. Hali ni mbaya,” anasema kwa huzuni.

Mkulima mwingine, Faraja Mussa Makame, anasema mavuno yamepungua mwaka hadi mwaka kutokana na ukataji wa mikoko.

“Serikali inapaswa kuanzisha miradi ya kurejesha uoto wa asili na kupambana na athari hizi,” anasema.

Mtumwa Abdallah Mohamed anasema zamani alikuwa akivuna magunia 10 ya mpunga kwa ekari moja, lakini sasa anapata gunia moja pekee.

“Hatuna pa kwenda, tunaendelea kulima sehemu zilizobaki. Serikali ije na suluhisho la kudumu,” anasema Mohamed.

Fatuma Hamisi Salum anasema licha ya kutumia mbegu bora na mbolea, mavuno yameendelea kuwa hafifu.

“Tunaomba Serikali na wadau wa mazingira watusaidie kurejesha mashamba yetu,” anasema.

Shughuli za kibinadamu zasababisha uharibifu

Haji anasema uharibifu wa mikoko unatokana na upanuzi wa mashamba na uchimbaji wa mchanga, akisisitiza kuwa sheria zichukue mkondo wake dhidi ya waharibifu wa mazingira.

Masika naye anasema jamii imehamasishwa kupanda mikoko kurejesha uoto wa asili, huku halmashauri ikifanya doria.

Nchinji anapendekeza doria hizo ziongezwe na adhabu kali zitolewe kwa wanaokata mikoko kinyume cha sheria.

Akizungumzia uchimbaji wa mchanga maeneo ya Pemba, Makame anasema hali hiyo inaenda sambamba na ukataji miti, kunakoongeza kasi ya kuingia kwa maji chumvi, hivyo kuharibu zaidi mashamba.

Mtaalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi, Paul Kyando, anasema njia bora ya kukabiliana na ongezeko la maji ya bahari ni kutumia njia za asili.

“Upandaji wa miti ya mikoko ni njia endelevu zaidi kwa sababu hupunguza kasi ya mawimbi ya bahari. Kujenga kuta au kingo mara nyingi hufanya tatizo lihamie maeneo mengine,” anafafanua.

Anaongeza kuwa si kila aina ya mikoko inakua katika mazingira yale yale, hivyo ni muhimu kufanya tafiti za kina kabla ya upandaji ili kuhakikisha matokeo chanya.

“Mikoko ipo ya aina nyingi, mingine huota majini, mingine pembezoni. Ni lazima wataalamu washiriki ili kupata ufanisi,” anasema.

Mwalim Khamis Mwalim, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazingira Zanzibar, anakubaliana na hoja hiyo, akisema taarifa kutoka tafiti zitasaidia Serikali kupanga miradi ya kudumu kama upandaji wa mikoko, ujenzi wa kingo na mabwawa ya maji.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Farhat Ali Mbarouk, anasema utafiti uliofanywa mwaka 2019 kwa ufadhili wa UNDP ulibaini athari za mmomonyoko wa fukwe, kuongezeka kwa chumvi na maji kujaa visiwani Unguja na Pemba.

Kwa mujibu wa Mbarouk, maeneo yaliyoathirika zaidi ni Nungwi, Mkokotoni, Bumbwini, Michamvi, Jambiani na Kisakasaka kwa upande wa Unguja, huku Pemba ikihusisha Msuka, Gando, Micheweni, Wingwi, Tovuni, Kwa Kingoji na Kisiwa Panza.

Anasema mradi mpya wa kukabiliana na tabianchi katika Kiongwe Kidogo utatekelezwa kwa miaka mitatu kwa gharama ya Dola milioni moja za Marekani (sawa na Sh2.5 bilioni). Mradi huo utahusisha ujenzi wa kingo, mabwawa, elimu kwa jamii na miradi mbadala ya kipato.

Mbarouk anasema Serikali imesaini pia mkataba na kampuni ya Global Network kufanya tathmini ya kina kuhusu udhaifu wa mazingira visiwani, baada ya awali kufanya tathmini katika eneo la Jambiani.

Anabainisha kuwa baadhi ya vyanzo vya maji navyo vimeanza kuchafuliwa na chumvi, jambo linaloathiri upatikanaji wa maji salama kwa matumizi ya binadamu.

Kwa sasa miradi ya Eco-system Based Adaptation na Green Legacy Initiative inaendelea kutekelezwa, ikilenga kupunguza athari za tabianchi kupitia ushiriki wa jamii, taasisi na sekta binafsi katika upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.