Wanafunzi 898,755 kufanya mtihani kesho, waaswa kuepuka udanganyifu

Dar es Salaam. Wanafunzi wa kidato cha pili takribani 898, 755 wanatarajia kufanya mtihani wa upimaji wa kitaifa (FTNA) kesho Novemba 10, 2025, hadi Novemba 20,2025 katika shule za sekondari 6,238 Tanzania Bara.

Kati ya wanafunzi hao waliosajiliwa kufanya mtihani huo 889,266 ni wanafunzi wa shule ambapo wavulana ni 396,383 sawa na asilimia 44.57 na wasichana ni 492,883 sawa na asilimia 54.43.

Kwa upande wa wanafunzi wa Kujitegemea 9,489 waliosajiliwa, kati yao wavulana ni 4,454 sawa na asilimia 46.94 na wasichana ni 5,035 sawa na asilimia 53.06.

Pia wanafunzi 4,390 wenye mahitaji maalumu wamesajiliwa kati yao, wenye uoni hafifu ni 1,674, wasioona ni 144, uziwi 999, ulemavu wa viungo 1,374 na wenye ulemavu wa akili ni 199.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Said Mohammed, wanafunzi 2,267 watafanya upimaji wa masomo ya amali kwa mara ya kwanza kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023 na Mtaala ulioboreshwa, na wanafunzi 886,999 watafanya mtihani kwa kutumia mtaala wa zamani.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa maandalizi yote kwa ajili ya kuendesha upimaji wa kidato cha kili yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za upimaji pamoja na nyaraka zote muhimu zinazohusu upimaji huo, katika halmashauri/manispaa zote nchini.

Pia maandalizi yote kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu yamefanyika ipasavyo.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Profesa Said Mohammed. Picha na Mtandao



“Kamati za mitihani za mikoa na halmashauri zimefanya maandalizi yote muhimu ikiwa ni pamoja na kutoa semina kwa wasimamizi wa upimaji na kuhakikisha kuwa mazingira ya vituo vyote ni salama.”

“Aidha, kamati za mitihani zimeweka mikakati ya kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu,” imeeleza taarifa hiyo.

Vilevile inatoa wito kwa kamati hizo kuhakikisha  kuwa usalama katika vituo vyote vya mitihani unaimarishwa na vinatumika kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na Necta.

Pia wasimamizi wa mitihani wamehimizwa kuzingatia kanuni za mitihani na miongozo waliyopewa kwa kufanya kazi ya usimamizi kwa weledi, umakini na uadilifu wa hali ya juu ili kila mwanafunzi aweze kupata haki yake.

“Wasimamizi wahakikishe wanafunzi wote wanafanya upimaji kwa muda uliopangwa na katika hali ya utulivu, na kuhakikisha wenye mahitaji maalumu wanapata haki zao za msingi.”

“Baraza linawataka wamiliki wa shule kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani na hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa upimaji huu,” imeeleza taarifa hiyo.

Vilevile imetoa onyo kwa wanafunzi kujiepusha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wakati wa upimaji huo kwani atakayebainika atachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za mitihani.

“Baraza linaamini kuwa walimu wamewaandaa vizuri katika kipindi chote cha miaka miwili, hivyo ni matarajio ya baraza kuwa wanafunzi watafanya upimaji kwa kuzingatia kanuni za mitihani,” imesisitiza taarifa hiyo.