Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wenyeviti wa Serikali za mitaa wakishinda udiwani kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imesema inasubiri taarifa rasmi ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kubaini walioshinda ili mitaa husika ifanye uchaguzi mdogo.
Tamisemi inayosimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa, ambao msimu huu ulifanyika mwaka 2024 imesema wale wote waliokuwa wenyeviti wa Serikali za mitaa na wameshinda udiwani, watalazimika kujiuzulu nafasi hizo ili mitaa waliyokuwa wakiiongoza ifanye uchaguzi kujaza nafasi hizo.
Baadhi ya wenyeviti wa mitaa katika wilaya kadhaa za Dar es Salaam na Pwani walijitosa kuwania udiwani na baadhi yao wameibuka kidedea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 huku wakiendelea kusalia kwenye nafasi zao za awali.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 (Revised Edition 2002) Kifungu cha 60(2) mwenyekiti wa Serikali ya mtaa hawezi kuwa diwani kwa wakati mmoja.
Sheria hiyo inaeleza kuwa, mwenyekiti wa mtaa akichaguliwa kuwa diwani, INEC au Tamisemi inapothibitisha, anafutwa kuwa mwenyekiti wa mtaa mara moja kwa mujibu wa Kanuni ya 8(1)(c) ya G.N. No. 283/2019 na kifungu cha 60(2) cha Cap. 288, mtu anayeshika nafasi ya kuchaguliwa ya ngazi ya juu (udiwani) anapoteza sifa ya kuendelea na nafasi ya chini (mtaa).
Kumekuwa na sintofahamu kwa baadhi ya wananchi kuhusu waliokuwa wenyeviti wao wa serikali za mitaa ambao ni madiwani wateule kwenye uchaguzi mkuu uliopita kuendelea na nafasi zao za awali.
Akifafanua hilo alipozungumza na Mwananchi leo Jumapili Novemba 9, 2025, Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru amesema kila aliyekuwa mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na kwenye uchaguzi uliopita ameshinda udiwani anapaswa kujiuzuru uenyekiti.
Amesema hivi sasa Tamisemi inasubiri taarifa ya INEC juu ya madiwani walioshinda kwenye uchaguzi mkuu ili wale waliokuwa wenyeviti wa Serikali za mitaa, mitaa yao ifanye uchaguzi mdogo kuziba nafasi.
“Hakuna mwenyekiti aliyekwenda kugombea udiwani akashinda na kubakia kwenye nafasi zote mbili, hiyo ni kinyume cha sheria, kila aliyeshinda udiwani anapaswa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti.
“Tunachosubiri kwa sasa ni taarifa ya INEC ya madiwani walioshinda ili mchakato mwingine uendelee kwenye mitaa ambayo wwnyeviti wake wamekuwa madiwani,” amesema.
Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (mitaa) G.N. No. 283 ya mwaka 2019, inasema mwenyekiti wa Serikali ya mtaa ni kiongozi wa mtaa, anayechaguliwa na wananchi wa mtaa husika na kazi yake ni kusimamia utendaji wa Serikali ya mtaa, kuongoza mikutano ya mtaa, na kutekeleza maelekezo ya halmashauri kupitia ofisa mtendaji wa mtaa.
Wakati diwani ni mjumbe wa baraza la halmashauri (manispaa, jiji au wilaya), anayewakilisha kata nzima, akihudhuria vikao vya baraza,anapitisha uamuzi na bajeti za halmashauri, ana wajibu wa usimamizi wa maendeleo ya kata nzima inayoweza kuwa na mitaa kadhaa au vijiji.
Kutokana na kanuni hizo, mwenyekiti wa mtaa aliyeshinda udiwani kuendelea kusalia kwenye nafasi zote mbili kunasababisha mgongano wa masilahi kwenye uwajibikaji wake.