Yanga kupangwa na waarabu Aziz Ki asema jambo

KIPINDI hiki ambacho mashabiki wa Yanga wanazidi kupasuka vichwa kuhusu kundi ambalo timu hiyo limepangwa katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kiungo wa zamani wa klabu hiyo Stephane Aziz KI ameizungumzia kwa mara nyingine timu yake hiyo ya zamani mara hii akisema bado ina uwezo wa kufanya makubwa.

Yanga ambao kwa ratiba ya mechi hizo sita za makundi iliyotoka, imepangwa kundi B pamoja na timu za Afrika Kaskazini ambazo ni Al Ahly ya Misri, JS Kabylie ya Algeria na AS FAR ya Morocco.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz Ki ambaye aliwahi kuwa mfungaji bora Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024, amesema ni wazi kabisa Yanga iko na wapinzani wagumu.

Amesema licha ya kikosi hicho kuwa kwenye kundi gumu, lakini wana uwezo wa kutoboa katika hatua hiyo kama tu watajipanga vizuri.

“Simjui kocha mpya aliyeletwa Yanga, lakini sina shida na ubora wa kikosi ambacho kipo, bila kusahau hesabu nzuri za mabosi wa klabu.

“Nimekuwa na mazungumzo mazuri na wachezaji na viongozi pia, hivyo sina shaka na mipango yao, kwani maandalizi wanayoendelea nayo, yananipa imani kubwa.

“Mashabiki nawasihi waendelee kuiunga mkono timu yao, mimi bado ni mfuatiliaji mzuri wa timu yangu ya zamani na ninaamini msimu huu itaweka rekodi nyingine mpya,” amesema.

Aziz Ki ambaye anaitumikia Wydad baada ya kuondoka Yanga msimu wa 2024-2025 ulipokuwa unakwenda ukingoni, amezungumzia kundi lao la Kombe la Shirikisho Afrika.

“Kundi letu sio rahisi wala gumu, lakini kwa ubora wa kikosi chetu tunataka kumaliza kileleni kwani naijua Azam vizuri.

“Lakini presha iliyopo Wydad tunatakiwa kucheza fainali, hayo yakiwa ni malengo ya uongozi wa klabu katika michuano hii ya Kombe la Shirikisho.

“Kikosi chetu kina wachezaji wakubwa kama kikiendelea kuboreshwa zaidi, ila kuhusu kundi tulilopo hatuna shaka,” amesema Aziz Ki.

Katika Kombe la Shirikisho, Wydad iko kundi B, ikiwa na AS Maniema United ya DR Congo, Azam FC (Tanzania) na Nairobi United (Kenya).

Wydad itanzia nyumbani Novemba 23, 2025 dhidi ya Nairobi United, huku siku hiyohiyo Azam FC ikiwa DR Congo kukabiliana na Maniema. Aziz KI anakumbukwa zaidi na mashabiki wa Yanga kutokana na mchango wake mkubwa klabuni hapo tangu alipojiunga nayo msimu wa 2022-2023 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast ambapo msimu huo alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger na kupoteza kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa 2-2. Mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 1-2, ugenini ikashinda 0-1.

Pia msimu wa 2023-2024, alikuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kilichocheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza, kisha 2024-2025 Yanga ikaishia makundi Ligi ya Mabingwa Aziz Ki akiwemo.

Katika misimu yote hiyo, Yanga imeshinda Ligi Kuu Bara na Kombe la FA. Pia mataji mengine kama Ngao ya Jamii na Kombe la Muungano.