Yanga yaishusha Simba, ikiizamisha KMC

YANGA imempiga KMC Kireno kwa kuichapa mabao 4-1 ikiishusha Simba katika  msimamo wa Ligi Kuu Bara angalau kwa wiki kadhaa wakati ligi ikienda mapumziko.

Yanga imefikisha pointi 10 baada ya kushinda mechi zake tatu na kutoa sare moja, ikiwarudisha Simba hadia nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa, sawa na Pamba Jiji iliyo nafasi ya tatu.

Hadi mapumziko timu hizo zilitoka zikiwa mzani sawa baada ya Yanga kutangulia kupata bao dakika ya 36 kupitia kiungo Maxi Nzengeli, aliyegongeana vizuri na mwenzake Pacome Zouzoua.

YANG 02


Hata hivyo, bao hilo likadumu kwa dakika sita pekee kwani lilisawazishwa dakika ya 42 na mshambukiaji Daruwesh Saliboko akimalizia mpira uliotemwa na kipa Djigui Diara kufuatia shuti la Rashid Chambo kufuatia shambulizi la adhabu ndogo.

Yanga ikapata bao la pili dakika ya kupitia kiungo wake Pacome Zouzoua dakika ya 73 akitumia krosi ya kazi nzuri ya beki wake wa kulia Israel Mwenda.

Wakati KMC wakiduwaa wakajikuta wakiruhusu mabao mawili mfungaji akiwa Andy Boyeli dakika za 81 na 90+3

YANG 01


Kuna mambo yameanza kubadilika kufuatia ujio wa kocha Pedro Goncalves ambapo Yanga jana ilionyesha kupiga pasi za haraka wachezaji wakigusa mpira na kukimbia.

Yanga ilikuwa imara ikionyesha pia kasi ya kuutafuta mpira mara baada ya kuupoteza hatua ambayo inarudisha ubora wa kikosi hicho.

Mashabiki wa Yanga ambao awali walikuwa wanachukia soka la timu yao, walionekana kufurahia namna kikosi chao kinavyocheza.

Kwa sasa Yanga inarudi kujiandaa kwa mechi za kimataifa za Ligi ya Mabingwa Afrika ikitarajiwa kuvaana na FAR Rabat ya Morocco Novemba 22 mjini Zanzibar kabla ya kuifuata JS Kabylie ya Algeria katika mechi ya pili ya Kundi B.