Biashara ya kimataifa EAC yapaa katika robo ya pili ya 2025

Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imerekodi ongezeko la biashara ya bidhaa za kimataifa katika robo ya pili ya mwaka 2025, ikisisitiza uimara wa kanda na ushindani unaokua katika masoko ya kimataifa.

Taarifa ya EAC kwa vyombo vya habari imenukuu Jarida la Takwimu la EAC kuwa jumla ya biashara iliongezeka kwa asilimia 28.4 yenye thamani ya Dola za Marekani 38 bilioni kutoka dola 29.7 bilioni katika robo ya mwaka wa 2024.

Mafanikio hayo yalichochewa zaidi na mauzo ya nje ambayo yaliongezeka kwa asilimia 40.5 yenye thamani ya dola 18.6 bilioni, ikionyesha ongezeko la mahitaji ya kimataifa ya bidhaa za EAC, huku uagizaji ukikua kwa asilimia 18.8 wenye thamani ya dola 19.6 bilioni.

“Matokeo yake nakisi ya biashara ilipungua kwa kiasi kikubwa kutoka dola 3.2 bilioni hadi dola 0.9 bilioni ikiashiria uboreshaji mkubwa katika usawa wa biashara ya nje,” imesema taarifa hiyo.

Biashara na nchi zingine za Afrika iliongezeka kwa asilimia 43, yenye thamani dola bilioni tisa ikichangia asilimia 24 ya jumla ya biashara huku biashara ya ndani ya EAC ikikua kwa asilimia 24.5 yenye thamani ya dola bilioni tano, ikiwakilisha asilimia 12 ya jumla ya biashara.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa EAC iliimarisha uhusiano wake wa kibiashara na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini Mashariki (Comesa) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC),  ambazo zilichangia asilimia 10 hadi 15 mtawalia kwenye biashara za kikanda katika maeneo mengine.

Aidha, mauzo ya nje yaliendelea kutoka China, Falme za Kiarabu, Afrika Kusini, Hong Kong na Singapore ambazo kwa pamoja ziliingiza asilimia 63 ya jumla ya mauzo ya nje, kutoka asilimia 40 mwaka mmoja uliopita.

Wakati nchi za Malaysia na Afrika Kusini zilisajili ukuaji wa juu zaidi wa robo mwaka, bidhaa tano bora za mauzo ya nje ni shaba, mawe ya thamani, metali, kahawa, chai na madini ambayo yalichangia asilimia 80  ya jumla ya mauzo ya nje ikilinganishwa na asilimia 77 katika robo ya pili ya mwaka 2024.

Pia China ilibaki kuwa chanzo kikuu cha uagizaji, ikichangia dola tano bilioni ambayo ni sawa na asilimia 24 ya jumla huku Falme za Kiarabu, India, Afrika Kusini na Japan pia ziliendeleza rekodi nzuri  zikichangia zaidi ya nusu ya bili ya uagizaji.

Bidhaa muhimu zilizoagizwa kutoka nje zilijumuisha petroli zenye thamani ya dola bilioni nne, mashine yenye thamani ya dola bilioni mbili, magari dola 1.5 bilioni, plastiki na bidhaa za chuma na chuma, zikionyesha uwekezaji unaoendelea katika miundombinu, viwanda na nishati.

“Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itaendelea kukuza mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, kuongeza thamani na kukuza ustawi wa pamoja katika nchi wanachama,” imeeleza taarifa hiyo.

Kuhusu masharti ya fedha, Jarida linabainisha kuwa viwango vya riba vya muda mfupi viliongezeka katika nchi nyingi wanachama wa EAC katika robo ya pili ya mwaka 2025, isipokuwa Kenya ambako kiwango cha bili ya hazina ya siku 91 kilipungua kwa pointi 70 za msingi hadi asilimia nane.

Jarida linaonyesha kuwa kiwango cha mikopo kilipungua kwa Kenya na Tanzania huku Uganda ikirekodi ongezeko kubwa zaidi la pointi 140 za msingi.

Viwango vya amana vilipungua au vilibaki thabiti kwa nchi nyingi wanachama isipokuwa Tanzania iliyorekodi ongezeko la pointi 70 za msingi.