Dar es Salaam. Takwimu zikionyesha zaidi ya asilimia 34 ya vifo vyote nchini, vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza (NCDs). Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya ndani na kisukari, Profesa Kaushik Ramaiya amesema kuna ongezeko la vifo vya mapema vitokanavyo na magonjwa hayo.
Magonjwa yasiyoambukiza ni pamoja na saratani, kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, afya ya akili, figo, selimundu na baadhi ya magonjwa ya njia ya hewa.
Takwimu za kidunia na za hapa nchini zinaonyesha idadi ya wagonjwa kuongezeka, ikikadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 34 ya vifo nchini Tanzania vinatokana na magonjwa hayo.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Novemba 10, 2025 Profesa Kaushik amesema takwimu hizo zinaakisi hali halisi ilivyo, kwani licha ya ongezeko la wagonjwa wa NCD vifo vingi hutokea kutokana na magonjwa kutotambulika mapema.
“Watu wengi wana magonjwa yasiyoambukiza wanaishi nayo bila kutambua na wanaendelea na tabia hatarishi ikiwemo ulaji usiofaa, watu wengi wana kisukari hawajui na wanakuja hospitali wakiwa tayari wameanza kupata changamoto zinazotokana na ugonjwa wanakuwa wamechelewa sana,” amesema.
Profesa Kaushik amesema changamoto kubwa ni uelewa wa jamii lakini pia kwa wagonjwa wenyewe wanapitia changamoto wanakotakiwa kuchukua dawa kunakuwa na matatizo kadhaa, hasa kama mgonjwa hakufuatiliwa katika usahihi wa utumiaji dawa unaosababisha athari kwa mgonjwa.
“Vifo vya mapema vya NCDs sasa vinatokea katika umri wa miaka 40-50 mpaka 60 hiki tunaita kifo cha mapema kwa kuwa umri wa mtu kuishi ni miaka 72,” amesema.
Hata hivyo amesema hali ya maisha inaweza kuchangia mtu kupata baadhi ya magonjwa ikiwemo kisukari kwa zaidi ya asilimia 40 mpaka 50.
Pamoja na hayo, Kaushik ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Shree Hindu Mandal ametaja hatua madhubuti ambazo zinatakiwa kufanyika ikiwemo elimu kwa jamii.
“Mtu akiona anapata kiu sana au anaanza kukojoa sana, uzito unapungua, anapata kidonda hakiponi anapaswa kwenda hospitali akapime kujua hali yake kiafya, kwani yaweza kuwa dalili za kisukari au matatizo mengine pia,” amesema Profesa Kaushik.
Kwa zaidi ya miaka 43 Profesa Kaushik Ramaiya (70) amekuwa akitoa huduma katika kliniki ya kisukari Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hindu Mandal kama daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya ndani na kisukari.
Takwimu zinaonyesha zaidi ya asilimia 34 ya vifo vyote nchini, vinatokana na magonjwa yasiyoambukiza, ambazo ni ongezeko la asilimia 1 kutoka zile za kwenye ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2022 iliyoonyesha magonjwa yasiyoambukiza yalichangia asilimia 33 ya vifo nchini.
Ongezeko hili linaonyesha kuwa mzigo wa NCDs unaongezeka kwa kasi nchini, wataalamu wakitaja hutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha kama vile ulaji usio bora, matumizi ya tumbaku na pombe, ukosefu wa mazoezi, na ongezeko la uzito kupita kiasi (obesity).
Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Jumatatu, Novemba 10, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Afya, Roida Andusamile imeeleza takwimu za kidunia na za hapa nchini zinaonyesha idadi ya wagonjwa kuongezeka, inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 34 ya vifo nchini Tanzania vinatokana na magonjwa hayo.
Kwa kuwa dalili za magonjwa hayo huchelewa kutambulika na yanaweza kuzuilika, Wizara ya Afya inawahimiza wananchi kufanya uchunguzi mara kwa mara ili kuyagundua mapema na kuanza matibabu.
“Tunahimiza kuzingatia mtindo bora wa maisha kwa kula mlo sahihi wenye virutubisho, kufanya mazoezi angalau dakika 30 kila siku, kuacha matumizi ya tumbaku na pombe na matibabu ya mapema ili kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza,” imeeleza taarifa hiyo.
Wiki ya magonjwa yasiyoambukiza nchini huadhimishwa wiki ya pili ya Novemba kila mwaka. Kwa mwaka 2025 maadhimisho haya yanaadhimishwa kuanzia Novemba 10 hadi 15, kwa lengo la kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya magonjwa yasiyoambukiza, umuhimu wa kuchukua hatua za pamoja katika kuyazuia na kuyadhibiti.
Kauli mbiu ya mwaka 2025 ni ‘Chukua hatua, dhibiti magonjwa yasiyoambukiza’, ambayo inasisitiza wajibu wa kila mmoja kuchukua hatua za kulinda afya yake na kusaidia jamii kuwa na maisha yenye ustawi.