Kisa ukame wa mabao, Dube apata mtetezi Yanga

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, David Molinga ‘Falcao’ amemkingia kifua Prince Dube aliyekumbwa na ukame wa mabao, kwa kusema hiki ni kipindi kifupi tu cha mpito hivyo atarejea kwenye makali yake.

Molinga aliyewahi kuwa kinara wa mabao wa Yanga msimu wa 2019/20 akiwa na mabao manane, amesema kama kuonyesha tayari Dube alishaonesha katika soka la Tanzania tangu akiwa na Azam kwake ni kati ya washambuliaji hatari.

Mkongomani huyo ambaye alikuwa uwanjani wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya KMC kwenye Uwanja wa KMC Complex, amesema amefurahishwa na namna ambavyo mashabiki wa timu hiyo walivyokuwa wakimsapoti.

“Kwa sapoti niliyoona anapewa ni rahisi kurudi kwenye kiwango chake, najua kwa sababu mimi nimecheza ile nafasi, hiki ni kipindi kigumu sana kwake kwa sababu anatamani kufunga na kuwapa raha wale ambao wamekuwa nyuma yake,” amesema.

DUB 01


Katika mechi tisa za mashindano yote, nne za Ligi ya Mabingwa, nne za ligi na moja ya Ngao ya Jamii, Dube amefunga bao moja tu huku akipoteza nafasi nyingi za wazi, hata hivyo ameendelea kuaminiwa na kupata nafasi ya kucheza mbele ya Andy Boyel ambaye alifunga mabao mawili dhidi ya KMC.

Bao hilo ilikuwa katika mechi ya kwanza ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Wiliete kwenye Uwanja wa Novemba 11 huko Luanda, Angola.

DUB 02


“Ujue kuna muda mshambuliaji anaweza asifunge lakini akarahisisha mipango ya timu katika kushambulia, kwangu bado anaweza kuendelea kuisaidia Yanga, bado ni mchezaji wa hatari. Wacha mashabiki wawe na subira,” amesema Molinga liyekumbushia hata yeye alianza vibaya Yanga hadi kocha wa enzi hizo, Mwinyi Zahera kumlia kiapo asipofunga zaidi ya 15 akatwe mkono.

Katika mechi nne za Ligi Kuu, Dube ameicheza jumla ya dakika 180, dakika 21 dhidi ya Pamba Jiji, dakika 10 dhidi ya Mbeya City, dakika 73 dhidi ya Mtibwa Sugar na dakika 76 dhidi ya KMC.

DUB 03


Huu ni msimu wa pili kwa Dube akiwa Yanga ndani ya msimu wake wa kwanza alifunga mabao 13 na kutoa asisti nane katika ligi.