KIUNGO nyota wa JS Kabylie ya Algeria, Babacar Sarr aliyewahi kukiwasha Msimbazi misimu miwili iliyopita, ameitaja Yanga ni timu ngumu na wanayoihofia katika Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na kuwa na wachezaji wenye uzoefu mkubwa.
Sarr na JSK wamepangwa kundi moja na Yanga, Al Ahly na FAR Rabat ya Morocco katika mechi za makundi za michuano hiyo ya CAF na timu hizo zinatarajiwa kukutana katika mechi za raundi ya pili, wawakilishi wa Tanzania wakiwa ugenini.
Kiungo huyo aliyesajiliwa na Simba kupitia dirisha dogo la msimu wa 2023-2024 na kuchemsha kabla ya kunyakuliwa na JS Kabylie, amesema wapo katika kundi gumu lakini lazima wapambane kuhakikisha wanashinda.
Amesema wapinzani hatari zaidi kwao ni wawili tu ambao ni Yanga na Al Ahly, lakini hawataingia kinyonge.
“Yanga ni timu ngumu, lakini naamini kwa ubora tulionao tunatakiwa kushinda mchezo wa kwanza kwetu Algeria. Kazi kubwa itakuwa mchezo wa marudiano kwani hautakuwa rahisi kwa kuwa tutakutana mwisho, itategemea na mechi zingine kabla ya hiyo,” amesema Sarr na kuongeza;
“Huwezi kuidharau Yanga kwa uzoefu walionao ingawa tunajua kwamba imepungua makali hivi karibuni, lakini shida ni kocha mpya ambaye uwezo wake unaweza kubadilisha mambo.”
Kiungo huyo aliyesajiliwa na Simba wakati timu hiyo ikifundishwa na Abdelhak Benchikha, kabla ya kocha huyo kumvuta tena JSK baada ya kuachana na Simba, hivi amekuwa tegemeo cha wababe hao wa Algeria na hivi karibuni amefunga bao la kwanza wakati timu hiyo ikishinda 4-1 mechi ya ligi dhidi ya El Bayadh kwa mabao 4-1.
Yanga itaanza karata za makundi Novemba 22 dhidi ya Far Rabat ya Morocco kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar kabla ya kuifuata JS Kabylie wiki moja baadae ugenini kisha kuja kucheza na Al Ahly mechi ya nyumbani na ugenini mfululizo Februari 2026.