Masai akiri Bara mziki mnene

NAHODHA wa Mtibwa Sugar, Oscar Masai amesema licha ya kupanda daraja wakitwaa taji la Championship wamekutana na ligi dume ambayo inawaamsha kujishikilia kabla ya kurudi walikotoka huku akitaja kuwa ujio wa kocha Yusuf Chippo utaongeza mbinu za kuiinua timu hiyo kiushindani.

Mtibwa Sugar imerudi Ligi Kuu baada ya kuangukia Championship kwa msimu mmoja na tayari katika mechi tano za ligi walizocheza wameshinda moja, sare mbili na vipigo viwili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Masai amesema walikuwa na msimu bora Championship lakini wamekosa mwendelezo huo Ligi Kuu, lakini wanaamini bado wana nafasi ya kufanya vizuri kutokana na aina ya kikosi walichonacho huku akimtaja kocha Chippo kuwa ataongeza nguvu katika benchi la ufundi.

“Msimu ni mgumu na hatujaanza vizuri, lakini haina maana kuwa ndio tumepoteza. Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwa muda uliopo na mechi zilizobaki ni mapema sana kuamini kuwa hatuwezi kuwa timu shindani. Naamini tuna muda wa kufanya masahihisho kwenye maeneo yenye upungufu,” amesema Masai na kuongeza;

“Ujio wa kocha mkuu ambaye licha ya kutangazwa mapema na kushindwa kuanza kazi kwa wakati kutokana na sababu binafsi, nafikiri sasa ni wakati wake kujenga timu na kuipambania iweze kufikia malengo.”

 “Hatutamani kurudi tulikotoka. Tuko tayari kuipambania Mtibwa Sugar irudi kwenye ushindani.”