WAKATI nyota ya kiungo Morice Abraham ikizidi kung’ara ndani ya Simba, kocha wa zamani wa kikosi hicho, Fadlu Davids ameshindwa kujizuia na kuweka wazi kama kuna kitu klabu hiyo imelamba dume msimu huu, ni kumsajili mchezaji huyo.
Morice aliyekuwa akiichezea RFK Novi ya Serbia, ametua Simba msimu huu akisajiliwa na Fadlu kabla ya kocha huyo kutimkia Raja Casablanca ya Morocco.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu amesema Morice ni mchezaji wa kutunzwa sana Simba kwani ana kipaji cha hali ya juu cha soka, ndiyo maana alimsajili baada ya kuridhishwa naye.
Fadlu ameiambia Mwanaspoti, hakutumia muda mrefu kuona kile kilichopo kwa kiungo huyo ila katika dakika chache alizompa mazoezini alionyesha uwezo wa tofauti.
“Nilitumia kipindi kimoja cha mazoezi niliyomualika Morice, lakini alinionyesha kiwango ambacho kilinifanya nimpitishe kama kiungo ninayetaka asajiliwe Simba. Ni mchezaji mwenye kipaji,” amesema Fadlu na kuongeza;
“Licha ya kwamba ni mchezaji mdogo ila ana kipaji kikubwa na anaeweza kuisaidia Simba kwa sasa na hata baadae kwani umri wake una faida kwa klabu hiyo na hata timu ya taifa, Taifa Stars.”
Morice amegeuka gumzo kwa uwezo alionao tangu aanze kuitumikia timu hiyo na mashabiki wameonyesha kumkubali na kuamini akipewa muda mrefu ataibeba timu kwa kipaji alichonacho.