Mtibwa Sugar yamgomea Mkenya | Mwanaspoti

MABOSI wa Mtibwa Sugar wameweka ngumu kwa kocha mpya wa kikosi hicho, Mkenya Yusuf Chippo aliyependekeza aje hapa nchini na msaidizi wake mmoja wa kufanya naye kazi, jambo ambalo limegonga mwamba na amejulishwa wengine atakutana nao akifika.

Chippo aliyeachana na Murang’a SEAL ya Kenya tangu Agosti 21, 2025, yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya kuiongoza kwa msimu huu, akishirikiana na Awadh Juma ‘Maniche’ aliyeipandisha daraja kwenda Ligi Kuu.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, umeliambia Mwanaspoti Chippo alipendekeza aje na kocha wa utimamu wa mwili ‘Fitness Coach’, ingawa mabosi wa kikosi hicho wamemgomea na kumtaka mwenyewe ili kupunguza pia gharama za kiuendeshaji.

Mwanaspoti linatambua suala la Chippo la kutaka msaidizi mwingine ndilo lililokwamisha kutua nchini kwa muda uliotakiwa, ingawa amekubaliana na alichoambiwa na uongozi na kuanzia sasa atatua Tanzania kwa lengo la kukifundisha kikosi hicho.

Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru amesema yapo mambo kadhaa yaliyokwamisha kocha huyo kutua nchini kwa muda uliotakiwa, japo kwa sasa kila kitu tayari kimekamilika na mashabiki wa timu hiyo watarajie ujio wake kuanzia wiki hii.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua mbali na suala la Chippo kuhitaji kuja na kocha wa utimamu wa mwili ambao ulisababisha dili hilo kuchelewa, ila suala lingine lilikuwa ni kucheleweshewa kutumiwa tiketi ya ndege na uongozi ya kutua Tanzania.

Sababu za Mtibwa kumkomalia Chippo ni baada ya kutozwa faini ya jumla Sh20 milioni na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), kwa kosa la kuanza msimu huu na kucheza mechi nne bila ya kocha mkuu mwenye ujuzi kwa mujibu wa Kanuni ya 77:33 (1,2,3).

Kiujumla Mtibwa imecheza mechi tano za Ligi Kuu Bara chini ya Awadh Juma ‘Maniche’, aliyeipandisha daraja ambaye hakidhi vigezo vya kusimamia benchi la ufundi kama kocha mkuu, jambo linalowafanya mabosi wa timu hiyo kupambana kumpata Chippo.

Chippo anakumbukwa na mashabiki wengi hasa baada ya kukiongoza kikosi cha Ulinzi Stars kutwaa mataji matatu mfululizo ya Ligi Kuu ya Kenya ‘KPL’ kati ya 2003 na 2005 na kuhudumu akiwa kocha msaidizi wa Harambee Stars kuanzia 2008 hadi 2011.

Kibarua cha kwanza kwa Chippo aliyezifundisha pia timu mbalimbali za Tanzania zikiwemo za Pamba Jiji, Coastal Union na TRA United zamani Tabora United, kitakuwa dhidi ya KMC, mechi itayopigwa Novemba 25 kwenye Uwanja wa KMC Complex.