Na Mwandishi wetu, Amboni-Tanga
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inatarajia kuendelea kuimarisha huduma za utalii katika mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga ili yaweze kuvutia watalii wengi kutoka maeneo mbalimbali duniani.
Akizungumza na watumishi wa kituo hicho kaimu Meneja wa Uhusiano kwa umma wa mamlaka hiyo, Afisa Uhifadhi Mkuu Hamis Dambaya amesema kuwa malengo ya kuboreshwa kwa huduma katika mapango ya Amboni yanatokana na mwelekeo mpya wa mamlaka hiyo ya kutaka kuongeza mapato na kutanua wigo wa vivutio vya utalii.
“Ndani ya Mapango tumeweka miundombinu ya taa, njia ya kutembelea wageni, mifumo ya TEHAMA na mazingira ya kupumzika wageni wanaotembelea Mapango haya, barabara ya kuja eneo la Mapango zinapitika vizuri na ujenzi wa geti umekamilika, tutaendelea na jitihada mbalimbali za maboresho ili eneo hili livutie wageni wengi zaidi” alisema Dambaya.
Miongoni mwa huduma zitakazoboreshwa katika eneo hilo ni pamoja na barabara ya kuingia mapango hayo na uanzishwaji wa mazao mapya ya utalii.
Mapango ya Amboni yaliyopo mkoani Tanga ni moja ya kivutio kikubwa cha utalii kutokana na kuwepo kwa miamba ya asili ambayo inatokana na historia ya kuumbwa kwa dunia.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Hifadhi ya Mapango ya Amboni Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza Ramadhan Rashid, eneo hilo hutembelewa na wastani wa wageni 18,000 kwa mwaka huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kutokana na uboreshaji wa miundombinu ya utalii pamoja na mifumo ya malipo







