Simulizi ya mizimu ya mganga na mauaji ya muuguzi mstaafu KCMC – 4

Moshi. Jana katika mfululizo wa simulizi ya mauaji ya muuguzi mstaafu wa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Patricia Ibreck yaliyofanywa na mganga wa jadi, Omary Mahmoud Rang’ambo, tuliwaletea ushahidi wa mtoto wa marehemu, Wende Mrema.

Katika ushahidi wake alioutoa mbele ya Jaji Safina Simfukwe wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, tuliishia pale mganga akisafisha mazingira ya nyumba baada ya kumuua na kumzika Patricia nje ya eneo la nyumba yake.

Wende alieleza namna alivyomsikia mganga huyo akisema kuwa, mizimu ilikuwa imefanikiwa kumsafirisha Patricia na kumtaka mtoto kuingia katika chumba cha mama yake na kufanya usafi, ndipo alihisi harufu ya ubani.

Leo tunakuletea sehemu ya mwisho ya ushahidi wake na wa mashahidi wengine.

Wende aliieleza Mahakama kuwa, Omary alimtaka ampe fedha nyingine kama gharama za kumtibu mama yake ili aweze kuondoka Moshi na alihitaji kati ya Sh20 milioni na Sh25 milioni, hivyo akalazimika kuuza shamba lake lingine.

 Alifanikiwa kupata mnunuzi aliyempa Sh10 milioni kwa kuwa,  hakuwa na uwezo wa kumlipa Sh25 milioni, hivyo alichukua fedha hizo na kumpa Omary aliyeondoka asubuhi.

Wende aliiambia Mahakama kuwa, aliendelea kumsumbua Omary akitaka kufahamu mama yake anaendeleaje na alimhakikishia kuwa, mama yake yuko salama na yeye anachotakiwa ni kuendelea kumtafutia pesa.

Alieleza kuwa, Machi 2021, viongozi wa kijiji walimfuata na kumuuliza mama yake yuko wapi; aliwaambia yuko India kwa matibabu na aliwadanganya kwa kuwa,  Omary alimpiga marufuku kuwaeleza kuwa amechukuliwa na mizimu.

Kwa mujibu wa Wende, Omary alimwambia endapo angetoa siri hiyo, angekufa na kuongeza kuwa, Omary alimpiga marufuku kwenda eneo lile walilompeleka mama yake kwa kuwa, kuna mizimu inamlinda, hivyo asiende hadi amwambie.

Ndipo Desemba 2021, maofisa wa polisi walimfuata na kumtaka awaeleze mahali alipo mama yake, aliwaeleza kuwa mizimu ya Omary ilikuwa imemchukua na inamtibu na aliamua kusema ukweli ili maofisa hao wamsaidie mama yake.

Wende alikuwa hafahamu mahali alipo Omary, isipokuwa aliwaeleza kuwa mganga mwenzake aitwaye Waziri anajua alipo, ndipo akawapeleka polisi hadi Korogwe ambako Waziri alikamatwa na polisi.

Shahidi wa nane, Mussa Liali aliyekuwa mwenyekiti wa Kijiji cha Rau, alieleza namna Machi 2022 alivyopokea taarifa za kutoweka kwa Patricia, kushirikiana na polisi na alivyoshiriki katika mchakato wa kufukua mabaki ya mwili wa Patricia.

Kichwa kilitenganishwa na kiwiliwili

Shahidi wa 10, Dk Alex Mremi ambaye ni daktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC, alieleza namna alivyoshiriki katika kazi ya kufukua mwili wa Patricia kutoka kwenye shimo na kuufanyia uchunguzi.

Alieleza kuwa, shimo alilokuwa amezikwa mama huyo lilikuwa na urefu wa kama meta moja na ndani ya shimo walikuta jambia, shuka ya kulalia na blanketi na kwamba jambia, lilikuwa na nywele, matone ya damu na mchanga.

Pia, walikuta mabaki ya mwili wa mtu mwanamke, mashuka na blanketi vyote vilikuwa na damu na fuvu lilikuwa na alama ya kukatwa na kitu chenye ncha kali na mwili huo ulikuwa umeharibika kutokana na kukaa zaidi ya miezi 10.

Dk Mremi alibaini kiini cha kifo kilitokana na kuvuja damu nyingi kulikosababishwa na kuchinjwa na kufafanua kuwa, hiyo ilitokana na kichwa kutenganishwa na kiwiliwili, matone ya damu kwenye shuka na blanketi na jambia lenye damu.

Shahidi huyo alieleza kuwa, kupinda kwa mkono wa mama huyo kunaashiria alikuwa akijitetea na kwamba, kama marehemu asingekuwa na majeraha, kusingekuwepo na damu katika mashuka ya kulalia, blanketi na nguo zake.

Kwa upande wake, shahidi wa 12, Stesheni Issa mwenye namba E.8872 aliyekuwa mpelelezi wa kesi hiyo, alieleza namna walivyopata taarifa za kutoweka kwa Patricia, kupeleleza na kukamata mtuhumiwa mkuu.

Baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha ushahidi wa mashahidi wao, Mahakama ilimuona mshitakiwa ana kesi ya kujibu.

Mganga alivyojitetea kortini

Katika utetezi wake, kwanza alianza kwa kulikataa jina lake la pili linaloonekana kwenye nyaraka za Mahakama akisema ni Mohamed na sio Mahmoud na akaelezea kwa kirefu shughuli inayomwingizia kipato na namna alivyokamatwa.

Alikanusha kutenda kosa la mauaji ya kukusudia ya Patricia na kusema ni mashtaka ya kutungwa yaliyochangiwa na kutoelewana kati yake na Wende baada ya kumfuma Wende akiwa na mwanamume mwingine chumbani kwake.

Kutokana na kitendo hicho, walivunja mahusiano, Wende alianza kumfuatilia ili kurejesha uhusiano na alipokataa kurudiana naye, Wende alimtishia kuwa, atamfanyia kitu ambacho hatakaa akisahau maishani mwake.

Hata hivyo, wakati akiulizwa maswali ya dodoso na wakili wa Serikali, Edith Msenga alikiri kuwa majina ya Omary Mahmoud Rang’ambo yalikuwa ni miongoni mwa mambo ambayo hayakubishaniwa wakati wa usikilizwaji wa awali.

Baada ya kumaliza kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili katika shauri hilo, Jaji Simfukwe alisema hoja kuu inayohitaji kuamuliwa na Mahakama ni kama upande wa mashitaka ulikuwa umeweza kuthibitisha shitaka pasipo kuacha shaka.

Jaji Simfukwe alisema kanuni kuu ya sheria za jinai, imeupa upande wa mashitaka jukumu la kuthibitisha shitaka linalomkabili mshitakiwa na viwango vya kuthibitisha shitaka hilo ni lazima lithibitishwe pasipo kuacha mashaka yoyote.

Alieleza kuwa, katika shitaka la mauaji, upande wa mashitaka ni lazima uthibitishe kwamba kuna mtu alikufa, kifo chake hakikuwa cha kawaida, mshitakiwa ndiye anawajibika na mauaji hayo na alifanya mauaji kwa nia ovu.

Katika kesi iliyopo mbele yake, Jaji alisema mganga huyo wa jadi anahusishwa na mauaji hayo kwa kuegemea vitu vitatu ambavyo ni kanuni ya yeye kuwa mtu wa mwisho kuwa na marehemu, ushahidi wa mazingira na maelezo yake ya onyo.

Jaji alisema hakuna ubishi, Patricia alikufa na kifo chake hakikuwa cha kawaida.

Katika kujibu hoja zingine, Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa sita (Wende)  wa Jamhuri, unaelezea namna mshitakiwa alivyompa Patricia dawa za kienyeji na alipopoteza fahamu, mshitakiwa alimtaka amletee jembe na shoka.

Mbali na vitu hivyo, lakini alimtaka alete na vitu vingine ambavyo kwa ajili ya kusafisha eneo hilo ili kuruhusu mizimu kuwepo na baadaye usiku Omary, alimtaka Wende ashirikiane naye kumbeba mama yake na kumpeleka nje ya nyumba.

“Hapo shahidi huyo wa sita akaamriwa aondoke kurudi chumbani kwake bila kuangalia nyuma anakotoka na pia azime taa zote. Baadaye akamwambia mama yake amechukuliwa na mizimu kwa ajili ya kwenda kumtibu,”alieleza Jaji.

“Inasikitishwa kwamba shahidi huyo wa sita alikuwa anamwamini sana mshitakiwa kama mganga wao wa jadi. Aliamini kila kitu alichoambiwa. Mshitakiwa alikuwa anawajibika kueleza aliachanaje achanaje na marehemu.”

Jaji akaongeza katika uchambuzi wake kuwa,  mshitakiwa alikanusha kutenda kosa hilo la mauaji na kumtuhumu mtoto wa marehemu kuwa ndiye alimtengenezea kesi hiyo kwa kuegemea mahusiano yao ya kimapenzi.

Usikose kufuatilia simulizi hii katika Gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii