TRA ILALA YAKABIDHI SH. MILIONI 30 KWA VIKUNDI VYA WAJASIRIAMALI

::::::::

Dar es Salaam,

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kodi Ilala, imekabidhi kiasi cha Sh. Milioni 30 kwa vikundi 15 vya wadau wa biashara kutoka mkoa huo wa kodi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda ya kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali aliyotoa Septemba 27, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dawati maalumu la Uwezeshaji Biashara kwa mkoa wa Dar es Salaam. 

Fedha hizo zimekabidhiwa leo tarehe 10.11.2025 na Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi Ilala, Bi. Eva Raphael kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za TRA mkoa wa Ilala na kueleza kuwa wameamua kuviwezesha vikundi hivyo ili viendeleze na kukuza biashara zao ikiwa ni miongoni mwa madhumuni ya kuanzishwa kwa dawati hilo maalum la kuwezesha biashara.

“Tunawashukuru sana kwa ushirikiano mzuri ambao mmekuwa ukiutoa kwa TRA na kuwa mabalozi wetu wa wazuri wa kueleza kazi zinazofanywa na TRA kwa jamii” amesema Bi. Eva.

Bi. Eva amevitaja vikundi vilivyonufaika kuwa ni Soko la Ilala, Soko la Zingiziwa, Soko la Chanika, Soko la Msongola, Soko la samaki Ferry,Soko la Kisutu,Soko la Mnadani Pugu,Soko la Gongolamboto,Soko la Buguruni Kwa Simba, Soko la nyamachoma machinjioni,Soko la Kinyerezi,Soko la Segerea,Umoja wa soko la Kimanga,Ushirikisho wa Umoja wa madereva wa pikipiki na bajaji Mkoa wa Dar es salaam na Soko la Kigogo.

Kwa upande wa Vikundi hivyo Katibu msaidizi wa soko la Pugu Mnadani Bw. Felix Chilumate amemshukuru Kamishna mkuu kwa kuwatambua wafanyabiashaa wadogo na kuendeleza kujenga Imani na wafanyabiashara ili wazidi kukua na kutambulika

Naye Mwenyekiti wa Soko la samaki Ferry Bw. Nasoro G Mbaga aliishukuru TRA kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogo wadogo na kuanzisha Dawati maalumu la uwezeshaji Biashara pamoja na kuwapatia kishika mkono ambayo itawasaidia katika kuongeza mtaji wa biashara zao.

Katika mgawanyo wa fedha hizo kila kikundi kimepatiwa Sh. Milioni Mbili.


= = = = = = =