TRA Ilala yakabidhi Sh30 milioni kwa vikundi 15 vya wafanyabiashara wadogo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa kikodi Ilala, imekabidhi Sh30 milioni kwa vikundi 15 vya wadau wa biashara kutoka mkoa huo wa kodi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda ya kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali.

Mwenda alitoa ahadi hiyo  Septemba 27, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa dawati maalumu la uwezeshaji biashara kwa Jiji la Dar es Salaam.

Fedha hizo zimekabidhiwa leo Novemba 10, 2025 na Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi Ilala, Eva Raphael kwa niaba ya Mwenda,  katika hafla iliyofanyika kwenye ofisi za TRA Mkoa wa Ilala na kueleza kuwa wameamua kuviwezesha vikundi hivyo, ili viendeleze na kukuza biashara zao ikiwa ni miongoni mwa madhumuni ya kuanzishwa kwa dawati hilo maalumu la kuwezesha biashara.

“Tunawashukuru sana kwa ushirikiano mzuri ambao mmekuwa ukiutoa kwa TRA na kuwa mabalozi wetu wa wazuri wa kueleza kazi zinazofanywa na TRA kwa jamii,” amesema Eva.


Eva amevitaja vikundi vilivyonufaika kuwa ni Soko la Ilala, Soko la Zingiziwa, Soko la Chanika, Soko la Msongola, Soko la samaki Ferry, Soko la Kisutu, Soko la Mnadani Pugu, Soko la Gongolamboto, Soko la Buguruni Kwa Simba, Soko la Nyamachoma machinjioni, Soko la Kinyerezi, Soko la Segerea, Umoja wa Soko la Kimanga, Umoja wa madereva wa pikipiki na bajaji Mkoa wa Dar es salaam na Soko la Kigogo.

Katibu msaidizi wa soko la Pugu Mnadani Felix Chilumate amemshukuru Kamishna Mwenda kuwatambua wafanyabiashara wadogo na kuendeleza kujenga imani nao itakayowawezesha  kukua na kutambulika.

Naye Mwenyekiti wa Soko la Samaki Ferry, Nasoro Mbaga ameishukuru TRA kwa kuwatambua wafanyabiashara wadogowadogo na kuanzisha dawati maalumu la uwezeshaji biashara pamoja na kuwapatia fedha hizo zitakazowasaidia  kuongeza mtaji wa biashara zao.

Katika mgawanyo wa fedha hizo kila kikundi kimepatiwa Sh2 milioni.