Uwekezaji MUST watajwa kuchochea ongezeko la udahili, wataalamu

Mbeya. Uongozi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), umesema uwepo wa miundombinu bora na ya kisasa itachochea ongezeko la udahili na kuibua wataalamu wenye ujuzi na kufungua fursa za ajira na uchumi kwa wanafunzi na walimu.

MUST ni miongoni mwa vyuo vikuu na kati nchini vilivyopata mradi wa elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) kwa usimamizi na uratibu wa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya makabidhiano ya majengo mapya kupitia mradi wa HEET kampasi za Mbeya na Rukwa, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Aloys Mvuma amesema miundombinu hiyo itaongeza ufanisi zaidi.

Amesema matarajio ya chuo ni kutoa mafunzo bora kumuandaa mhitimu kuwa mbobezi, kwa kuwa atajifunza kwa nadharia na vitendo kutokana na uwepo wa majengo na vifaa bora vya kisasa kumuwezesha mwanafunzi kuwa imara kitaaluma.

Mamaku Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya Prof Aloys Mvuma (wa pili kutoka kulia) akiwa na viongozi wa Chuo hicho wakati wa hafla hiyo. 



“Kwa sasa tuna wataalamu bobezi, majengo bora na ya kisasa, hivyo tunaenda kufikia dira yetu, tunayo miundombinu ya kujifunza na kufundishia, maabara, karakana na mitaala yenye kujibu mahitaji ya soko la ajira.

“”Huu ni mtaala ambao unakwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya kiuhandisi na kutoa fursa kwa vijana kujiajiri na kuajirika ambapo tayari Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) imeupitisha na mwaka ujao wa masomo tutaanza kuutumia,” amesema Profesa Mvuma.

Profesa Mvuma ameongeza kuwa hadi sasa chuo hicho kimeweka mazingira rafiki kwa baadhi ya viwanda ili wanafunzi wanaosoma kwa nadharia wapate ujuzi kwa vitendo na kwamba MUST, wamejipanga kuwa mahiri kwenye sayansi na teknolojia.

“Niwaombe wanafunzi watunze vema miundombinu hii, watumishi tumieni fursa hii kutengeneza bunifu mbalimbali ili kujiingizia kipato kitaasisi na mtu mmojammoja,” amesema.

Kwa upande wake, mkandarasi wa jengo la taaluma, kampasi ya Mbeya, Ensheng Xiong ameishukuru Serikali kwa ushirikiano walioutoa tangu kuanza kwa ujenzi wa mradi huo mwaka 2023 hadi kukamilika kwake, mwaka huu.

Amesema kwa sasa jengo hilo lipo tayari kwa matumizi, akieleza kuwa matarajio ni kuona vijana wakipata elimu bora na kulisaidia Taifa.

Mamaku Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya akipokea funguo kuashiria kukamilika kwa majengo hayo kampasi ya Rukwa na mkandarasi Faraji Seleman kutoka kampuni ya Til construction Ltd.



“Tunashukuru kwa ushirikiano uliotuwezesha kufikia mafanikio haya, matarajio yetu ni kuona vijana wakipata elimu katika mazingira bora ili kuliwezesha Taifa katika nyanja ya sayansi na teknolojia,” amesema Xiong.

Akitoa taarifa ya mradi wa jengo la taaluma katika kampasi ya Mbeya, mhandisi mkazi, Joseph Mkisi amesema jengo hilo limegawanyika katika makundi mawili yaliyogharimu zaidi ya Sh29 bilioni.

“Mradi huu una majengo manne, la kwanza ni  la taaluma, karakana, kitovu cha ubunifu na uhuishwaji wa teknolojia pamoja na mandhari yote,” amesema na kuongeza:

“Kwa ujumla ujenzi huu ulikuwa katika mgawanyo wa sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ni taaluma na mandhari iliyogharimu takribani Sh16 bilioni huku roti ya pili ikigharimu takribani ya Sh13 bilioni,” amesema.

Kwa upande wake, Rasi wa chuo hicho, kampasi wa Rukwa, Profesa Asheri Mwideke amesema wanashukuru kwa mradi huo mkubwa na wa kimkakati.