Waitara aonya udanganyifu utekelezaji miradi ya Tanapa

Arusha. Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Jenerali George Waitara amewataka wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya shirika hilo kufuata maadili, uadilifu na weledi katika kazi.

Waitara ambaye ni Mkuu wa Majeshi mstaafu amesema hayo leo Jumatatu, Novemba 10, 2025 jijini Arusha wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni Tanzu ya Uwekezaji ya Tanapa (Tanapa Investment Ltd – TIL)

Jenerali Waitara amesema Bodi ya Wadhamini haitasita kuchukua hatua za kisheria endapo kutabainika udanganyifu au ukiukwaji wa taratibu katika utekelezaji wa miradi.

“Ninachoomba ni udanganyifu usiwepo kabisa maana mnajua kitakachofuata ni hatua za kisheria na kinidhamu, ikiwemo kuvunjwa kwa bodi yenu hivyo sitarajii jambo hilo litokee,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara, akizungumza kabla ya uzinduzi wa bodi ya TIL



Mbali na hilo, amesisitiza bodi hiyo kuzingatia uwazi na uadilifu katika utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo.

Aidha, ameipongeza bodi mpya ya TIL kwa kuteuliwa na kuwataka kuimarisha uongozi wa kitaalamu na kuongeza ubunifu katika uwekezaji utakaoleta tija kwa shirika na taifa kwa ujumla.

“Twende tukasimamie kwa uwajibikaji na uadilifu huku tukijenga taswira chanya ya kampuni katika sekta za umma na binafsi, tukitekeleza miradi inayooana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na falsafa ya uhifadhi endelevu,” amesema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi wa Tanapa, Mussa Kuji amesema shirika linaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo kubuni mazao mapya ya utalii ili kufikia malengo ya Taifa ya kuwa na watalii milioni nane ifikapo 2030 kutoka milioni tano wa sasa.


Amesema Tanapa inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, mageti na madaraja ili kupunguza vikwazo vinavyowakumba watalii, hasa msimu wa mvua zinazosababisha uharibifu wa miundombinu.

Naye Mtendaji Mkuu wa TIL, Dk Richard Matolo amesema kampuni imejipanga kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya ukandarasi kwa kutumia wataalamu wenye uwezo na vifaa vya kisasa.

“TIL tuna wataalamu wenye uzoefu mkubwa na vifaa vya kisasa. Tunaahidi kufanya kazi zenye ubora wa hali ya juu,” amesema.

Amesema kampuni ya TIL ni tanzu ya Tanapa iliyoanzishwa kwa madhumuni ya kutekeleza miradi ya ndani ya shirika kwa gharama nafuu na pia kufanya miradi ya nje kama sehemu ya kuongeza mapato.

“Hii itasaidia miradi yetu kutekelezwa kwa wakati bila vikwazo vyovyote tena kwa gharama nafuu na uimara wa hali ya juu tofauti na kutegemea watekelezaji wa nje,” amesema.