Na; OWM (KVAU) – Nairobi
Wajasiriamali wa Tanzania wamepongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwawezesha kushiriki Maonesho ya 25 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), maarufu kama Nguvu Kazi au Jua Kali, yanayoendelea jijini Nairobi, Kenya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wajasiriamali hao wamesema Serikali imewasaidia kugharamia usafiri pamoja na mizigo yao, jambo ambalo limeongeza ari na hamasa ya kushiriki kwa wingi katika maonesho hayo.
“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha kufika Nairobi. Hii ni fursa ya kipekee kwetu kukuza biashara zetu na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wa nchi nyingine,” amesema mmoja wa washiriki.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika Jumuiya ya Afrika Mashariki upande wa Tanzania (CISO–Tanzania), Josephat Rweyemamu, amesema Serikali imeendelea kuratibu ushiriki wa wajasiriamali hao ili kuwawezesha kutangaza bidhaa na huduma zao nje ya mipaka ya nchi.
Maonesho hayo ya 25 yamebeba kaulimbiu isemayo: “Miaka 25 ya Ujumuishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki: Kuendeleza Ubunifu na Minyororo ya Thamani ya Kikanda kwa Biashara Ndogo na za Kati Shindani kuelekea Maendeleo Endelevu.”






