Watanzania zaidi ya 300 watoa taarifa za ukiukwaji wa haki TLS

Dar es Salaam. Kwa siku tano pekee, zaidi ya Watanzania 300 wamejitokeza kutoa taarifa kwa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuhusu matukio ya ukiukwaji wa sheria na uvunjaji wa haki za binadamu yaliyotokea kuanzia Oktoba 28, 2025, na baada ya uchaguzi mkuu.

Kati ya makundi yaliyotoa taarifa, familia za watu wanaodaiwa kufariki dunia ndizo zimejitokeza kwa wingi, ingawa TLS imesisitiza kuwa inahitaji taarifa kutoka kwa makundi yote yaliyokumbwa na matukio ya kupotea, kujeruhiwa au kuathirika kwa namna yoyote ili kupata takwimu sahihi zitakazoiwezesha kuishauri Serikali kuchukua hatua stahiki.

Uhamasishaji wa wananchi kutoa taarifa hizo unatokana na tamko la TLS lililotolewa Novemba 5, 2025, likiwataka Watanzania wote wenye taarifa kuhusu ukiukwaji wa sheria au haki za binadamu tangu Oktoba 28 mpaka sasa kuwasilisha taarifa hizo ili kusaidiwa kisheria.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Novemba 10, 2025, Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, amesema licha ya watu hao kuwasilisha taarifa zao, bado mwamko ni mdogo kutokana na hofu na upotoshaji unaoenezwa kwamba kutoa taarifa ni usaliti.

“Ni zaidi ya watu 300 wametuma taarifa zao, lakini bado kuna hofu kubwa. Wengine wanadanganywa kwamba wasilete taarifa kwa TLS kwa madai eti ni ‘wasaliti’. Huo si ukweli, tunachofanya ni kutetea haki na sheria,” amesema Wakili Mwabukusi na kuongeza:

“Tunataka kujua ni wangapi wamekufa, wamejeruhiwa au wamepotea. Hatuwezi kukaa kimya, tunahitaji hatua za uwajibikaji zichukuliwe kwa maslahi ya wote,” amesema.

Hata hivyo, amesema bado hawajapata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wananchi na akahimiza kila aliyeathirika au mwenye taarifa kufika ofisini au kuwasiliana na TLS kwa ajili ya msaada wa kisheria.

“Tunatoa msaada wa kisheria bure, hakuna malipo yoyote. Tunachohitaji ni taarifa sahihi kuhusu mtu, yuko wapi au kama amepelekwa mahakamani ili tumsaidie kupata wakili mwenye sifa,” amesema.

Kwa mujibu wa Wakili Mwabukusi, jitihada hizo zinafanywa kwa ushirikiano na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanaokabiliwa na kesi zinazohusiana na matukio hayo wanapata msaada wa kisheria bila ubaguzi.

Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amethibitisha ushirikiano huo na kusema mitandao hiyo imeanza maandalizi ya kutoa msaada wa kisheria kwa watu zaidi ya 400 waliofikishwa mahakamani katika mikoa mbalimbali nchini.

“Tunajiandaa kutoa tamko la pamoja na TLS. Tumejipanga kuwapatia mawakili wote wanaokabiliwa na kesi mahakamani na wale wanaoendelea kufunguliwa mashtaka. Huu ni wajibu wa kikatiba,” amesema Olengurumwa.

Kwa upande wake, Wakili Fulgence Massawe kutoka LHRC amesema wameanza kutoa msaada wa kisheria kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakishikiliwa na polisi, wengi wao sasa wamefikishwa mahakamani.

“Kwa aina ya makosa wanayotuhumiwa nayo, ni lazima wapate uwakilishi wa lazima kwa mujibu wa sheria,” amesema Massawe.