Moshi. Tabia ya wanawake kulia wanapokerwa na jambo na kuzungumza wazi kuhusu hisia na changamoto zinazowakabili, imetajwa kuwasaidia kuepuka matatizo ya afya ya akili ikilinganishwa na wanaume, ambao mara nyingi hubaki kimya na kubeba matatizo yao kwa muda mrefu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Dk Kim Madundo, amesema tofauti za kijinsia katika namna watu wanavyokabiliana na changamoto za maisha zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa katika kuongezeka kwa matatizo ya afya ya akili kwa wanaume.
Ameyasema hayo leo Jumanne Novemba 11, 2025 wakati akitoa elimu ya afya ya akili kwa watendaji wa kata, vijiji, walimu, viongozi wa dini na wataalamu wa afya kutoka Moshi vijijini, iliyoandaliwa na shirika lisilo la kiserikali linalojishughulisha na shughuli za maendeleo ndani ya jamii (FTK), kwa kushirikiana na KCMC pamoja na wataalamu wa afya ya akili kutoka Uholanzi.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC), Dk.Kim Madundo
Amesema wanawake kwa asili ni wawazi zaidi katika kuonyesha hisia zao, husema wanapoumizwa na hata kulia wanapopata msongo wa mawazo, jambo ambalo huwasaidia kupunguza mzigo wa kihisia.
“Wanawake huwa na tabia ya kuonyesha hisia zaidi, kuwa na wasiwasi na hofu, na ni wepesi kulia. Wanaume wao mara nyingi huonyesha hasira lakini hubaki na changamoto zao moyoni kwa muda mrefu bila kushirikisha wengine,” amesema Dk Kim.
Amesema ukimya wa wanaume katika kushughulikia matatizo yao umekuwa chanzo kikubwa cha msongo wa mawazo, hali inayosababisha wengine kuingia kwenye ulevi wakidhani ni njia ya kujinasua, lakini ikigeuka kuwa suluhisho la muda mfupi lisiloondoa tatizo.
“Wapo pia watu wakimya na wapole wasiopenda kushirikisha changamoto zao. Kundi hili nalo liko kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata matatizo ya kisaikolojia,” ameongeza Dk Kim.
Akizungumza katika semina hiyo, Mchungaji Kiongozi wa Usharika wa TPC na Magadini, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), David Pallangyo, amesema kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na mafunzo kuhusu afya ya akili kwa kushirikiana na wataalamu wa saikolojia na walimu ili kusaidia kupunguza changamoto hizo.
Amesema wanawake huwa hawapati changamoto kubwa za kisaikolojia kwa sababu wanapoona jambo linawazidi, husema au kuliahivyo kupunguza maumivu ya ndani.
“Ni kweli wanaume wengi wanakumbwa na tatizo hili la afya ya akili kutokana na tabia ya kukaa kimya na kubeba mambo yanayowaumiza bila kushirikisha wengine. Ni muhimu sasa wakabadilika na kujenga utamaduni wa kusema au kuzungumza wanapokuwa na changamoto,” amesema.
Ameongeza kuwa, “Kusema au kulia ni uponyaji. Wanaume wengi hawafanyi hivyo, lakini kusema kunasaidia sana kupunguza msongo wa mawazo,” amesema Mchungaji Pallangyo, akieleza kuwa semina hiyo imekuja wakati muafaka kusaidia jamii ya TPC.
Daktari bingwa wa magonjwa ya afya ya akili kutoka nchini Uholanzi, Rolf Schwarz amesema wanaume na wanawake wote wanapata matatizo ya afya ya akili, wanatofautiana mazingira ya kupata changamoto hiyo.
“Wapo wenye uelewa kuhusu changamoto ya afya ya akili, lakini cha kufanya kukabiliana na tatizo hilo hawajui. Mahitaji ni makubwa hivyo tunawajengea uwezo ili waweze kuisaidia jamii kuondokana na changamoto hii.”
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Shirika la FTK, Lazaro Urio amesema walifanya utafiti mdogo na kubaini kuwa wengi wanaoanza kuonyesha dalili za matatizo ya afya ya akili hukosa msaada wa awali, kwa sababu viongozi wa karibu nao hawana uelewa wa kutosha wa kuwashauri au kuwaelekeza sehemu sahihi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Dk Juma Mombokaleo, amesema mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali na wadau katika kuimarisha huduma za afya ya akili nchini.
Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo, kuhakikisha elimu wanayoipata inatumika kubaini na kusaidia watu wenye changamoto hizo.