Dar es Salaam. Watanzania wawili wanasayansi kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara Health (IHI), Paul Mrosso na GloriaSalome Shirima wameshinda Tuzo ya Mtafiti Mdogo ya Marekani ya ASTMH (American Society of Tropical Medicine and Hygiene), mwaka 2025 huko Toronto, Ontario, Canada.
Tafiti walizoshinda zilihusu kubuni mbinu za kuongeza mafanikio ya kuzaliana kwa mbu wa Anopheles funestus katika maabara maalumu ya kufugia mbu, na kutafiti nyavu mpya za mbu kwa ajili ya kudhibiti malaria nchini Tanzania.
Wawili hao wanakamilisha idadi ya Watanzania wanne kuwahi kushinda tuzo hiyo, akiwemo Issa Mshani aliyeshinda mwaka 2023, na ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Profesa Fredros Okumu miaka 15 iliyopita ambaye ni Mtafiti Kiongozi IHI, pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland, Uingereza.
Tuzo hizo zimetolewa leo Jumanne, Novemba 11, 2025 katika mkutano wa ASTMH ulioanza Novemba 9 unaotarajiwa kumalizika Novemba 13 mwaka huu.
Paul Mrosso ni mwanasayansi kutoka IHI na mwanafunzi wa PhD katika Chuo Kikuu cha Glasgow, pamoja na GloriaSalome Shirima, mwanasayansi na mwanafunzi wa PhD, kutoka Chuo Kikuu Uswisi.
Katika mradi wake, Paul Mrosso alijikita katika kubuni mbinu za kuongeza mafanikio ya kuzaliana kwa mbu wa Anopheles funestus katika maabara maalumu ya kufugia mbu (insectary).
“Anopheles funestus ni mojawapo ya spishi hatari zaidi za mbu wanaosambaza malaria barani Afrika. Ni mbu mwenye uwezo mkubwa wa kueneza malaria, lakini ni vigumu sana kuzalishwa kwenye mazingira ya maabara. Changamoto hii imekuwa ikiwafanya wanasayansi duniani kote washindwe kuchunguza kwa undani tabia na biolojia yake, jambo linalozuia maendeleo katika utafiti na udhibiti wa malaria,” amesema Mrosso.
Kupitia utafiti wake, Mrosso aligundua njia bora za kuboresha hali ya mwanga inayotumika katika maabara hizo, na hivyo kuongeza kwa kiasi kikubwa mafanikio ya kuzaliana kwa spishi hiyo ya mbu.
Mafanikio hayo yamefungua milango mipya kwa tafiti za malaria, yakiruhusu wanasayansi kuelewa vizuri zaidi mbu huyu hatari. Mchango huu wenye athari kubwa katika sayansi ndio uliompatia Mrosso tuzo hiyo.
Gloria alifanya utafiti kuhusu kuelewa nyavu mpya za mbu kwa ajili ya kudhibiti malaria nchini Tanzania.
Malaria bado ni tatizo kubwa katika maeneo mengi ya Afrika kwa sababu mbu wameanza kuwa sugu kwa kemikali zinazotumika kwenye nyavu za kawaida za kuzuia mbu, na nyavu hizo pia hazidumu kwa muda mrefu.
“Wanasayansi tumebuni aina mpya ya wavu wa mbu unaochanganya viuadudu viwili, chlorfenapyr na alpha-cypermethrin ili kufanya nyavu ziwe imara zaidi na zenye ufanisi mkubwa.
“Utafiti huu ulitumia mfumo wa kompyuta (simulation) kutabiri ufanisi wa nyavu hizi mpya nchini Tanzania ikilinganishwa na nyavu za kawaida na zile za “PBO” (nyavu zenye kemikali ya ziada inayosaidia kushinda usugu wa mbu),” amesema Gloria.
Amesema watafiti walichunguza njia tofauti za kusambaza nyavu, kama kampeni za kugawa kwa wingi au kupitia kliniki za afya za watoto, na walizingatia maeneo yenye viwango tofauti vya hatari ya malaria.
“Matokeo yalionyesha kuwa nyavu hizi mpya zinazuia wagonjwa wengi zaidi wa malaria kuliko za kawaida au za PBO kwa wastani, zinazuia visa 16 zaidi kwa kila mtu baada ya hatua moja ya kugawa nyavu kwa wingi. Pia, zinaendelea kupunguza maambukizi ya malaria kwa kipindi cha hadi miaka mitatu, hasa zinapotolewa kwa watoto,” amesema.
Matokeo ya utafiti wake yanapendekeza kuwa kutumia nyavu hizi za kizazi kipya katika maeneo sahihi kunaweza kusaidia kulinda watu wengi zaidi dhidi ya malaria, na kuwasaidia watunga sera kupanga matumizi bora ya rasilimali.
Tuzo hizi hutolewa kwa mtu kuwasilisha kwa njia ya maongezi mbele ya majaji matokeo ya kazi yake ya utafiti aliyoifanya mwenyewe kwa kiasi kikubwa akiwa ndiyo mtendaji mkuu katika kazi hiyo, ambayo hujumuisha wataalamu kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Heshima hii hutolewa kwa watu wanaofanya utafiti kwa kujitegemea na kuwasilisha matokeo yao mbele ya jopo la majaji, wakiwa waandishi wakuu na watekelezaji wakuu wa kazi hiyo.