BAADA ya kuambulia pointi moja katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam, winga wa Namungo FC, Helbert Lukindo amesema bado wana kazi ngumu kusaka matokeo mazuri kutokana na ugumu wa ligi hiyo msimu huu, hivyo wanaendelea kupambana.
Namungo haijawa na matokeo mazuri msimu huu kwani katika mechi sita ilizocheza imekusanya pointi sita sawa na wastani wa pointi moja kila mechi, inakamata nafasi ya 10 kwenye msimamo.
Kama haitoshi, kati ya mechi sita hizo ni moja tu ilimaliza dakika 90 bila kuruhusu bao ilipoifunga Tanzania Prisons bao 1-0, Septemba 21, 2025, huku nyingine tano ikiokota mpira wavuni, hali inayowapa mtihani kuondokana na matokeo hayo.
Katika mechi iliyopita Novemba 9, 2025, Namungo ikiwa nyumbani, ilitoshana nguvu ya bao 1-1 dhidi ya Azam, ambapo inatarajia kushuka tena uwanjani kuikaribisha Dodoma Jiji, Novemba 21, 2025 huko Ruangwa mkoani Lindi.
Matokeo ya mechi zingine za timu hiyo ni; Namungo 1-1 Pamba Jiji, Simba 3-0 Namungo, JKT Tanzania 1-1 Namungo na Mashujaa 1-0 Namungo.
Lukindo alisema bado hawajawa na mwanzo mzuri wa matokeo kutokana na ugumu wa ligi kwa timu zote msimu huu, akieleza kuwa hawakati tamaa badala yake ni kuendelea kupambana.
Alisema matokeo ya mechi iliyopita licha ya hesabu zao kutaka pointi tatu kukwama, lakini sare hiyo haikuwavunja moyo na sasa wanajipanga kutofanya makosa watakapowakabili Dodoma Jiji ili kujiweka pazuri.
“Ligi imeanza kwa ugumu, hatuwezi kukata tamaa kwa kuwa bado ni mapema na uwezo tunao kwa mchezaji mmoja mmoja, lolote linawezekana, kimsingi ni kutopoteza mwelekeo,” alisema Lukindo.
Staa huyo aliyewahi kukipiga Mbao na KenGold, ameongeza kuwa licha ya kikosi kuwa na mastaa wengi, lakini ameweza kuaminiwa kuwa kikosi cha kuanza, akiahidi kuwa kila mechi kwake ni kupambana kulinda namba.