CHAMA la nyota wawili wa Tanzania, FC Masar ya Misri, limefufua matumaini ya kuisaka nafasi ya nusu fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake baada ya juzi Jumanne kuitandika 15 De Agosto mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Suez Canal nchini Misri.
Nyota hao ni Hasnath Ubamba ambaye amekuwa kikosini hapo kwa takribani msimu wa tatu sasa tangu alipojiunga nayo akitokea Fountain Gate Princess na mwingine ni Violeth Nickolaus aliyesajiliwa msimu huu akitokea Simba Queens.
Wawili hao wamecheza mechi zote mbili za kundi A wakiiwezesha timu hiyo kukaa kileleni mwa msimamo ikiwa na pointi nne, mechi ya kwanza ilitoka sare tasa dhidi ya AS FAR Rabat (W).
Sasa baada ya ushindi huo mnono, Novemba 15, 2025, Masar inashuka tena kwenye Uwanja wa Suez Canal mjini Ismailia kusaka angalau pointi moja dhidi ya USFAS Bamako ambayo itaipeleka hatua ya nusu fainali kwa mara ya pili mfululizo.
Hiyo inatokana na hivi sasa pointi nne ilizonazo, ikipata moja tu itafikisha tano ambazo hazitafikiwa na USFAS Bamako iliyo nafasi ya tatu kwa sasa ikikusanya pointi tatu. Kumbuka katika michuano hiyo yenye timu nane, kuna makundi mawili na kila kundi linatoa timu mbili za juu kufuzu nusu fainali.
Mwaka jana, Masar iliposhiriki michuano hiyo ilimaliza katika nafasi ya tatu baada ya kupokea kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya AS Far katika nusu fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Ben M’Hamed El Abdi El Jadida nchini Morocco.
Hivyo kama chama hilo litatinga tena nusu fainali msimu huu, Ubamba ataandika rekodi nyingine ya kuipelekea timu hiyo kwa mara ya pili mfululizo.
Kwa Violeth, kama Masr itavuka itakuwa mara yake ya pili kucheza hatua hiyo, mara ya kwanza alikipiga akiwa Simba Queens mwaka 2022 iliyomaliza nafasi ya nne baada ya kuondolewa na mabingwa wa zamani Mamelodi Sundowns kwa bao 1-0 nchini Misri.
Msimamo wa Kundi A unasomeka hivi; FC Masar inaongoza ikiwa na pointi nne sawa na AS FAR Rabat, USFAS Bamako ya tatu pointi tatu na FC 15 de Agosto haina kitu, zote zikicheza mechi mbili. Mechi ya mwisho FC Masar dhidi ya USFAS Bamako na AS FAR Rabat ikiikabili FC 15 de Agosto.