KIUNGO mshambuliaji wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo amewataja Crispin Ngushi wa Mashujaa na Ismail Aziz Kader anayecheza Fountain Gate kwamba anapenda aina ya uchezaji wao na huiga baadhi ya vitu vya kiufundi kwao.
Chobwedo aliyejiunga na TRA United msimu uliopita kwa usajili wa dirisha dogo akitokea KenGold alikocheza nusu msimu, alisema kabla ya kuanza kucheza Ligi Kuu, Ngushi na Kader ndiyo alikuwa anawafuatilia zaidi aina ya uchezaji wao.
“Ni wazalendo uwanjani, unaona wanavyojitolea kupambania timu, hilo lilikuwa linanivutia kuona ili ufanikiwe lazima ujitoe bila kuchoka,” alisema Chobwedo na kuongeza;
“Huu utakuwa msimu wangu wa pili kucheza Ligi Kuu, hivyo kupenda kujivunza kwa wengine kulifanya nisione ugumu wa kupambana na mazoezi binafsi kuwa sehemu ya maisha yangu ya kila siku, labda itokee niumwe ndipo nitapumzika.”
Alisema kabla ya kucheza Ligi Kuu, aliitumikia TMA Star ya Ligi ya Championship, huku akibainisha kwamba Ligi Kuu inahitaji mifumo, mbinu, akili na nguvu ili kufanikiwa.
“Mpira wa miguu unapaswa kujifunza vitu vipya kila wakati ili kuendana na sayansi ya kazi hiyo, ingawa msimu huu nauona mgumu kwangu, naamini kuna kitu kitaongezeka,” alisema Chobwedo aliyekiri pesa yake kubwa kuimiliki kwa mara ya kwanza ilikuwa Sh10 milioni.