Dk Mwinyi kutangaza Baraza la Mawaziri kesho

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi anatarajia kutangaza Baraza la Mawaziri kesho Alhamisi, Novemba 13, 2025 Ikulu Zanzibar.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Raqey Mohamed leo Novemba 12, 2025 imesema hafla hiyo itafanyika saa 4:00 asubuhi.

“Hafla hiyo itahudhuriwa na wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, ambapo Rais Mwinyi atalitangaza Baraza jipya la Mawaziri na Wizara zake,” imesema taarifa hiyo.

Imesema pia, Dk Mwinyi ataeleza mwelekeo na dira kuu ya uongozi wa baraza jipya katika kutekeleza vipuambele vikuu vya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Vipaumbele hivyo vitajikita katika uchumi wa buluu, uwekezaji, huduma za jamii, miundombinu na maendeleo jumuishi kwa wananchi.

Wateule hao wanatarajia kuapishwa Jumamosi Novemba 15 saa 8:00 mchana katika viwanja vya Ikulu Zanzibar. Hafla hiyo ya uapisho ni hatua muhimu katika kuanza rasmi safari ya kipindi cha pili cha serikali ya awamu ya nane.

Dk Mwinyi anaendelea kuiunda serikali yake baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikamtangaza mshindi wa kiti cha urais kwa kupata kura 448,892 sawa na asilimia 74.8.

Mshindani wake wa karibu kwenye mbio hizo za urais alikuwa, Othman Masound Othman maarufu OMO wa ACT-Wazalendo aliyeambulia kura 139,399 sawa na asilimia 23.22. OMO alikuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Baada ya ushindi huo, Novemba 1, 2025 aliapishwa kuwa Rais wa visiwa hivyo kumalizika miaka mitano kwa mujibu wa Katiba.

Rais Mwinyi ambaye anapeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tayari amekwisha kulizindua Baraza la Wawakilishi Novemba 10, 2025 ambalo lina idadi kubwa ya wawakilishi wa chama chake.

Uteuzi wa kwanza kufanya baada ya kuapishwa ni wa Dk Mwinyi Talib Haji ambaye alimteua Novemba 4, 2025 kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na alimwapisha Novemba 6, 2026.

Aidha, Rais Mwinyi ambaye huu ni muhula wake wa mwisho wa miaka mitano, amemteua tena na kumwapisha, Hemed Suleiman Abdulla kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.