BEKI wa KMC, Ismail Gambo amesema kwamba kikosi hicho kipo kwenye wakati mgumu baada ya kufungwa mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Bara msimu huu.
KMC ambayo imeanza msimu vibaya, inashika mkia ikiwa na pointi tatu katika mechi sita ilizocheza, huku ikishinda moja pekee, ikifunga mabao mawili na kuruhusu kumi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Gambo alisema ni mapema kusema msimu utakuwa mbaya licha ya kwamba wamekuwa na matokeo yasiyofaa yanayowaweka katika wakati mgumu kurudi kuwa sawa.
Alisema kuwa, kikosi hicho kwa sasa kiko kwenye wakati mgumu na presha kubwa kuanzia benchi la ufundi mpaka wachezaji.
“Kilichosalia ni kusonga mbele kutazama mechi ijayo dhidi ya JKT Tanzania, kwani tuna mechi nyingi bado za kucheza, kama tutaamua kusimama imara tena inawezekana kubadili hali hii.
“Kwa sasa tunataka kutuliza akili, mpaka mchezo ujao naamini tutakuwa na utofauti mkubwa, hivyo mashabiki wasitukatie tamaa,” alisema.
KMC tangu ilipoifunga Dodoma Jiji katika mechi ya kwanza msimu huu Septemba 17, 2025, haijaonja ushindi wala sare kwa takribani siku 58.
Novemba 21, mwaka huu, KMC iliyotoka kufungwa 4-1 na Yanga, itakutana na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge jijini Dar, huku wapinzani wao wakipoteza mechi ya mwisho kwa mabao 2-1 dhidi ya Simba.