Haki huinua taifa (Mithali 14:34), na haki na amani vinagusana (Zaburi 85:10). Wenye kutoa hukumu dhidi yetu na dhidi ya wengine watoe hukumu kwa haki (Qur’an 4:58) na haki ifanywe kipaumbele (Qur’an 16:90).
Tujitahidi kudumisha Tanzania ya uhuru, umoja na amani; zaidi tujenge Tanzania mpya yenye haki, usawa na furaha, misingi ya amani ya kweli.
Kufuatia yaliyotokea katika uchaguzi uliopita na athari zake kwa taifa, jambo la kwanza na la msingi kuliko yote ni kuponya nchi yetu na kutafakari njia sahihi ya kutoka tulipo. Kama alivyonukuliwa Rais Samia Suluhu Hassan: “Maandamano na vurugu husababisha maumivu na hayaleti manufaa kwa yeyote. Tuchague hekima, busara, upendo, uvumilivu, umoja na amani.”
Maneno haya yana uzito mkubwa na yanapaswa kuwa dira ya taifa letu katika kipindi hiki cha mpito na majonzi.
Wazungu wana msemo: “Justice must not only be done, but must also be seen to be done.” Yaani haki isitendwe tu, bali ionekane kutendeka. Kwa kuwa baadhi ya watu wameshtakiwa, ni muhimu wakatendewa haki bila upendeleo.
Tusiwe kama tenga la samaki, yaani kosa la mmoja linahesabiwa kuwa la wote. Mfano wa binti aliyejipatia riziki kwa kuuza barakoa, lakini akakamatwa na kushitakiwa kwa uhaini, unaonesha jinsi mfumo wa utoaji haki unavyopaswa kuangaliwa kwa makini ili kuepuka kuumiza wasiostahili.
Msemo mwingine unasema, ‘It takes two to tango,’ ukimaanisha kila mzozo una pande mbili, chanzo na matokeo.
Ikiwa serikali itashughulikia matokeo pekee bila kuchunguza mizizi ya tatizo, chanzo hicho kitaendelea kuchemka chini kwa chini. Wakati moshi unafuka, moto unazidi kusambaa, na siku ukilipuka, utasababisha madhara makubwa zaidi. Hivyo, ni busara serikali kushughulikia mizizi ya migogoro badala ya matokeo yake tu.
Vilevile, msemo wa “Don’t add insult to injury” unatukumbusha kwamba pale kunapokuwa na majeraha, tusiyazidishe kwa maneno au vitendo vinavyoongeza maumivu.
Uchaguzi huu umesababisha vifo, uharibifu wa mali na majeraha ya kihisia kwa Watanzania wengi. Ni wakati wa kutafuta tiba, si kuongeza vidonda. Tusiendelee kunyoosheana vidole au kufunguliana kesi za uhaini; badala yake, tujielekeze katika kuijenga upya roho ya taifa letu.
Serikali inapaswa kuzingatia kutoa msamaha wa jumla kwa wote walioguswa na matukio haya, kwani maandamano si chanzo bali ni matokeo ya hisia na malalamiko yaliyopandwa kwa muda mrefu.
Ikiwa waandamanaji wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma nzito za uhaini, basi ili haki ionekane kutendeka, ni lazima pia wale waliohusika na matumizi ya nguvu kupita kiasi waliopiga, kuua au kushiriki vitendo kinyume cha sheria, nao wawajibishwe. Haki isiwe upande mmoja pekee.
Ushauri wangu ni kwamba tuendelee kupeana pole na kujifunza kutokana na yaliyotokea. Tuiombe serikali iwe tayari kufungua ukurasa mpya wa maridhiano ya kitaifa, ili damu na machozi ya Watanzania yasipotee bure. Msamaha wa kweli na uwajibikaji wa pande zote ndio msingi wa amani ya kudumu.
Nimalizie kwa maneno yale yale ya vitabu vitakatifu:
“Haki huinua taifa” (Mithali 14:34),
“Haki na amani vinabusiana” (Zaburi 85:10),
“Toeni hukumu kwa haki” (Qur’an 4:58),
na “Haki ifanywe kipaumbele” (Qur’an 16:90).
Tuidumishe Tanzania yetu ya amani, uhuru na umoja na tujenge Tanzania mpya yenye haki, furaha na upendo.