LICHA ya kukusanya pointi nane kwenye mechi sita walizocheza wakishinda mbili, sare mbili na vipigo viwili, Kocha Mkuu wa Mbeya City, Malale Hamsini amelia na washambuliaji na walinzi wa timu hiyo akiweka wazi kuwa hawana uwiano mzuri, hivyo ana kazi kubwa ya kufanya kuiweka timu hiyo kwenye ushindani.
Malale ambaye mechi mbili za mwisho amekusanya pointi moja baada ya kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons na sare ya mabao 2-2 mbele ya JKT Tanzania, ameliambia Mwanaspoti kuwa, ana kikosi kizuri ambacho kina upungufu mdogo anaoufanyia kazi.
Amesema pamoja na kuanza vizuri baada ya kurejea kushiriki Ligi Kuu Bara licha ya kutokuwa na wastani mzuri wa kushinda, kiwango cha washambuliaji na mabeki wake hakijamridhisha na ana kazi ya ziada kuwaweka fiti na kiushindani ili kujihakikishia nafasi ya kucheza tena ligi msimu ujao.
Amesema ikiwa ni mechi yake ya tatu kuwaongoza vijana hao, atahakikisha anawaweka katika mfumo anaoutaka ili timu hiyo ipate matokeo mazuri na kuwa ya ushindani.
“Timu imerejea kambini tangu Ijumaa ya wiki iliyopita, mimi ndio naenda Mbeya kuendelea kufanyia kazi mapungufu yaliyoonekana kwenye mechi sita tulizocheza hadi sasa ambazo nakiri kuwa ugumu upo lakini tuna kikosi ambacho kina uwezo wa kupambana.
“Hakuna kazi isiyo na changamoto, haya yanayoonekana sasa ni kawaida, tutafanyia kazi na kila mmoja atarudi kwenye mstari sahihi, lengo ni kuona timu inaonyesha ushindani na kuwa sehemu ya timu bora msimu huu licha ya kwamba ndio kwanza imerudi baada ya kushuka,” amesema Malale.
Mbeya City kwenye mechi sita ilizocheza imefunga mabao saba na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita, hivyo haina wastani mzuri kwenye kufunga na kuzuia.