Dar es Salaam. Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limetoa wito kwa Serikali kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa namna ya kujenga umoja wa kitaifa na utengamano wa kijamii.
Mbali na hilo, Kanisa hilo limeitaka Serikali kuwatendea haki raia wote waliopoteza maisha au walioathiriwa katika maandamano yaliyozaa vurugu wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Kanisa hilo limekwenda mbali, likisema matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa yeyote hayawezi kuleta baraka na neno la Mungu linaonya:“Hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu…tena wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi.”
Mkuu wa KKKT, Askofu Alex Malasusa amesema hayo kupitia taarifa yake kwa umma aliyoitoa leo Jumatano, Novemba 12, 2025 ikiwa na kichwa cha habari ‘Neno la KKKT kuhusu matukio ya wiki ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.’
Wito huo wa KKKT unawiana na ule uliotolewa kwa nyakati tofauti na viongozi wa Kanisa Katoliki Tanzania wa kulaani mauaji na matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi huku wakitaka kufanywa maombi, kujitathmini kama taifa na kusisitiza amani itakayozingatia haki.
Walitoa kauli hizo katika misa za kuwaombea walioathirika na vurugu hizo, wakiwamo waliopoteza maisha katika matukio hayo.
Katika misa ya kuwaombea marehemu iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu Dar es Salaam Novemba 10, 2025, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Juda Thadeus Ruwa’ichi, alisema yaliyotokea wakati wa uchaguzi Oktoba 29, 2025, yamelijeruhi na kupoteza heshima ya Taifa.
Alisema si tu taifa limepoteza heshima, bali limepoteza pia raia waliouawa kiholela.
“Katika simulizi zinazoendelea, wapo watu waliouawa wakiandamana, lakini adhabu ya kuandamana sio kifo cha risasi. “Wapo waliouawa wakiwa majumbani mwao, hilo halionyeshi sura ya Tanzania hata kidogo, na halina maelezo wala msamaha, ni chukizo mbele za Mungu,” alisema.
Aidha, Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Vernon Fernandes akizungumza Novemba 3, 2025 mara tu baada ya Samia Suluhu Hassan kuapishwa katika Uwanja wa Gwaride, Chamwino, Dodoma, alisema Taifa limegawanyika na mioyo ya watu imejeruhiwa kwa namna mbalimbali.
Alimwomba Rais Samia kulileta Taifa pamoja na kuiponya mioyo hiyo na kwamba alifanye hilo kuwa kipaumbele chake.
“Umepokea jukumu kubwa la kihistoria. Taifa limegawanyika na mioyo ya watu imejeruhiwa kwa namna mbalimbali. Ombi langu kwako kwa niaba ya umma wa Tanzania, ulilete Taifa pamoja na kuiponya mioyo hii, hili likiwa kipaumbele chako,” alisema.
Katika taarifa ya Askofu Malasusa amesema kanisa hilo limeguswa na kuumizwa na matukio hayo yasiyokuwa ya kawaida na kusikitishwa na matukio haya yaliyokosa utu, heshima na thamani ya binadamu. Kanisa linakemea matukio hayo yanayomchukiza Mungu.
“Kanisa linatoa wito kwa Serikali kusikiliza na kushughulikia malalamiko ya wananchi kwa namna ya kujenga umoja wa kitaifa na utengamano wa kijamii,” amesema.
Kiongozi huyo amesema: “Kanisa linatoa wito kwa Serikali kuwatendea haki raia wote waliopoteza maisha au walioathiriwa.”
Malasusa ambaye pia ni Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, amesema KKKT inatoa pole kwa jamii na familia zilizopoteza wapendwa wao kwa kuuawa au bado hawajapatikana bila maelezo ya kuridhisha.
“Baadhi ya familia hazijaweza hata sasa kuwapata ndugu zao waliouawa wakati wa vurugu hizo ili kuwafanyia mazishi kwa utaratibu wa kijamii na kiibada. Hali hii imeacha jamaa mbalimbali katika simanzi kubwa ya misiba na maombelezo yasiyoelezeka,” amesema Askofu Malasusa.
Amesema hakuna sababu yoyote inayotosheleza kueleza upotevu wa maisha na uharibifu wa mali na kanisa hilo litawaombea wafiwa wote, majeruhi, watu ambao bado hawajapatikana na wanaoshikiliwa bila hatia.
Amesema Kanisa la Mungu kwa upana wake linaungana kuomba toba na rehema kwa Mungu ili nchi yetu iliyoshuhudia umwagaji wa damu za watu ipate kuokolewa dhidi ya ghadhabu ya Mungu juu ya chukizo hili na ipate neema ya kurejea katika amani.
Kutokana na hilo, Askofu Malasusa amesema kanisa linatoa wito kwa washarika wake wote kuwa na maombi maalumu kwa wiki nzima kuanzia ibada zote za Jumapili ya Novemba 16, 2025.
“Kisha kila siku maombi yaendelee hadi Jumapili ya Novemba 23, 2025,” amesema akielekeza kwa siku za Jumapili, ujumbe wa kalenda utumike na kutoa utaratibu maalumu wa kutumia katikati ya wiki.
Kwa mujibu wa ratiba ya maombi Jumatatu yataongozwa na wanawake, vijana (Jumanne), Jumatano (wanaume), Alhamisi (vikundi vya kwaya), Ijumaa (vikundi vya fellowship) na vikundi vya Jumuiya vitaongoza maombo Jumamosi wakati Jumapili itakuwa siku ya kumshukuru Mungu.
Ameelekeza wanataaluma wote wa huduma ya ushauri kichungaji katika dayosisi zote za KKKT watumie muda huu kutoa tiba ya nafsi na roho kwa wote walioumizwa.