Kocha Malindi ataka rekodi mpya ZPL

KOCHA Msaidizi wa Malindi, Mohamed Salah ‘Richkard’ amesema mabadiliko iliyofanya timu hiyo msimu wa 2025-2026 yanalenga mambo makuu mawili ambayo ni kuuza wachezaji kimataifa na kuweka rekodi ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Amesema timu hiyo kwa sasa ina kiu ya kutwaa ubingwa wa ligi hiyo unaoshikiliwa na Mlandege, ili kuleta ushindani wa kimataifa katika soka la Zanzibar.

“Malindi ina hamu kubwa ya kuchukua ubingwa wa ZPL na ndio maana inafanya juhudi mbalimbali kuhakikisha hilo linatimia, ikiwa hatujafanikiwa Ligi Kuu, tutajipanga kuchukua Kombe la Shirikisho (FA Cup),” alisema Richkard.

Alisema awali mashabiki na wadau wa michezo waliibeza timu hiyo, lakini baada ya mechi mbili kila mmoja alishangazwa kuiona ikiwa na mabadiliko ambayo hawakutarajia kama yatakuwepo.

Pia alifafanua wachezaji waliopo sasa wanafuata misingi ya timu na wanathamini kazi kwani wanaamini kilichowafanya kubaki walipo ni kucheza mpira na kuiletea mafanikio timu hiyo.

Mbali na kufanya vizuri katika ligi, Richard amekuwa sababu mojawapo ya mashabiki wa timu hiyo kufika uwanjani kushuhudia burudani kutokana na aina ya ushangiliaji wake.

Hata hivyo, kocha huyo amesema hapendezwi kuiona timu hiyo ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ndio maana huwa anawahamisha wachezaji kufanya vizuri wakati wa mechi.

Kwa sasa Malindi inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ZPL ikicheza mechi saba, ushindi nne na sare tatu, ikivuna alama 15 nyuma ya vinara KVZ yenye 16. Malindi ndiyo timu pekee inayoshiriki ligi hiyo haijapoteza mechi msimu huu.