::::::
Na Mwandishi Wetu,
MAMLAKA ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) imetangaza kuanza kwa mchakato wa tuzo kwa watoa huduma bora na salama katika sekta ya usafiri ardhini kwa mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Mhandisi Habibu Suluo, alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya LATRA, Sura ya 413, kinachotoa jukumu kwa Mamlaka hiyo kuhamasisha ushindani wenye ufanisi miongoni mwa watoa huduma wanaodhibitiwa.
“Kupitia mfumo huu wa tuzo, tunalenga kuongeza ushindani wenye tija, ubunifu, usalama na ufanisi katika utoaji wa huduma za usafiri ardhini, sambamba na malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs 2030),” alisema Mhandisi Suluo.
Alifafanua kuwa tuzo hizo zinalenga kuboresha mazingira ya ushindani, kuchochea ubunifu na matumizi ya teknolojia, pamoja na kuimarisha huduma bora na salama za usafiri ardhini zinazozingatia mahitaji ya makundi maalum ya jamii.
Tuzo hizo zitatolewa katika Maadhimisho ya Kwanza ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini 2025, yatakayofanyika kuanzia Novemba 24 hadi 29, 2025, katika viwanja vya LATRA Makao Makuu, Tambukareli – Dodoma, huku shughuli za maonesho zikifanyika Mnazi Mmoja, Dar es Salaam na mikutano ya elimu ya usafiri ikifanyika JNICC.
Washiriki wa tuzo hizo wamegawanywa katika makundi manane, ikiwemo watoa huduma wa mabasi ya mikoani na nchi jirani, magari ya mizigo, magari maalum ya kukodi, madereva na wahudumu, mifumo ya tiketi na teksi mtandao, watoa huduma wa vifaa vya kufuatilia magari (VTD) na waandishi wa habari.
Vigezo vya washindi vitazingatia ubora wa huduma, matumizi ya teknolojia, utii wa sheria na kanuni, utunzaji wa mazingira na huduma endelevu. Kampuni kama New Force, BM One, Shabiby Line, USANGU Logistics, Uber, Bolt, FARAS na Twende Technologies zimeorodheshwa katika hatua ya tathmini.
Kwa mujibu wa LATRA, wananchi watapiga kura kupitia tovuti ya [www.latra.go.tz](http://www.latra.go.tz) au [www.tanzaniatransportweek.co.tz](http://www.tanzaniatransportweek.co.tz) hadi Novemba 20, 2025, huku waandishi wa habari wakihimizwa kuwasilisha kazi zao kupitia barua pepe [info@latra.go.tz](mailto:info@latra.go.tz) au WhatsApp 0681 300 800.





