Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameileza Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar ea Salaam kuwa amefikisha siku 216 akiwa rumande huku akiwasilisha hoja sita kupinga shahidi wa upande wa Jamhuri asitoe ushahidi wake akiwa ndani ya kizimba maalumu cha ushahidi wa siri.
Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusiana na kuzuia kufanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Anadaiwa akiwa raia wa Tanzania, tarehe hiyo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, huku akitamka na kuandika maneno ya kumshinikiza kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania.
Mshtakiwa huyo anadaiwa kwa kuthibitisha nia hiyo ya uasi alimshinikiza Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Tanzania kwa maneno aliyoyatamka na kuyaandika.
Leo Jumatano, Novemba 12, 2025 kesi hiyo iliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka, ambapo upande wa Jamhuri walidai wanae shahidi ambaye yupo kwenye orodha ya mashahidi ambao wanatakiwa kulindwa kwa kutotajwa jina lake, kazi yake wala eneo anakoishi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga ametoa taarifa hiyo mbele ya Jopo la Majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha, kutoka Mahakama Kuu Songea na Ferdinand Kiwonde, kutoka Mahakama Kuu ya Bukoba.
“Waheshimiwa majaji, kesi imeitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka na leo tunaye shahidi moja ambaye ni shahidi wa nne wa upande wa mashtaka, hivyo tupo tayari kuendelea na usikilizwaji,” amedai Katuga.
Katuga amemtaja shahidi huyo kuwa ni P11, ambaye katika orodha ya mashahidi wa Jamhuri ni shahidi ambaye anatakiwa kulindwa.
Baada ya Katuga kutoa mwelekeo huo, mshtakiwa alisimama na kupinga shahidi huyo asiote ushahidi wake akiwa ndani ya kizimba maalumu kilichotengenezwa kwa ajili ya mashahidi wanaolinda kutoa ushahidi wao eneo hilo.
Badala yake, Lissu amedai shahidi huyo anapaswa kutoa ushahidi wake katika kizimba cha wazi na sio kizimba kilicho funikwa maarufu kama kizimba cha boksi, huku akitaka sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwa na kanuni inayoelekeza shahidi huyo kutoa ushahidi wake katika kizimba kilichifunikwa.
Kutokana na hali hiyo, Lissu amewasilisha mapingamizi sita kupinga shahidi huyo kutoa ushahidi wake katika kizimba cha bosi.
Katika hatua nyingine, Lissu amedai yupo rumande kwa siku 216 na kwa kuwa kesi hiyo leo ulikuwa siku ya mwisho ya tarehe zilizokuwa zimepangwa kwa mujibu wa kikao cha Mahakama, ameomba mahakama itakapofanya kikao kingine cha kupanga tarehe ya kuendelea na kesi hiyo, basi wapange tarehe za karibu ili kesi hiyo iweze kuendelea kwa haraka kwa kuwa upande wa mashtaka bado wana mashahidi zaidi ya 25 ambao hawajatoa ushahidi wao.